Thursday, May 24, 2018

Unataka kuwa na furaha kwenye mahusiano?


Furaha haiji tu kwenye mahusiano. Furaha hutengenezwa na watu wenyewe walio kwenye mahusiano. Ukitaka kuwa na furaha katika mahusiano yako jitahidi kufanya yafuatayo:
A
Hakikisha unakuwa chanzo cha furaha yako mwenyewe. Ule usemi wa raha jipe mwenyewe hapa ndipo ninapoupenda zaidi. Ila lakini raha ya kupewa si ndiyo tamu zaidi? Kumbuka siyo jukumu la mpenzi wako peke yake kukupa furaha bali jukumu ni lenu wote. Ndiyo, mpenzi wako anaweza kujitahidi kwa udi na uvumba kuhakikisha unafurahi lakini itakuwa kazi bure kama juhudi hizo hautazifanya wewe mwenyewe pia. Achana na malumbano ambayo mwisho wake ni kuumizana na badala yake jaribu kuwa mwelewa, mpole na msikivu. Wakati mwingine unajua kabisa jambo fulani litaleta ugomvi lakini mtu unaamua tu kulianzisha. Ninachosema ni kwamba furaha yako ni muhimu sana kwenye mahusihano na jukumu la kuhakikisha unafurahi lipo mikononi mwako. Kumbuka ukijinyima furaha unajipunguzia hata muda wa kuishi halafu wanasema pia ukizira wenzio wala.
B
Timiza ahadi zako. Kama umeahidi kufanya kitu ama kumpa mpenzio zawadi ama kumpeleka sehemu fulani hakikisha unatimiza. Usipofanya hivyo utajikuta kwenye migogoro na kununiwa. Kama umeahidi kitu hakikisha unatimiza tena siyo mpaka ukumbushwe. Kama ulimwahidi kwenye birthday yake utamnunulia perfume basi hakikisha unanunua la siyo utakosa hata huduma zingine. Na pengine umeahidi ukagundua hutaweza kufanikisha toa taarifa mapema ili usimwache mwezio anakusubiri kwa hamu halafu unaingia mikono mitupu, hii inakera sana wakati mwingine unatamani kummeza mtu. Unaweza ukaona ni jambo dogo tu lakini nakuambia linachangia kwa kiasi fulani migogoro mingi kwanza huondoa uaminifu na humjima mwenzio furaha. Hivi nani asiyejua ule mkao wa kusubiria zawadi tena ambayo umeahidiwa kwa miezi kadhaa au pengine hata mwaka. Halafu mtu anaingia mikono mitupu, yaani unajikuta hutaki kuamini kwamba hamna zawadi basi utaisaka nakuambia hata mpaka kwenye soksi alizovaa. Ili kuepuka haya ya kutafuta zawadi kwenye soksi ukiahidi timiza ama sema mapema kwamba zawadi imeshindikana.
C
Kubali ukikosea. Umefanya kitu kwa kujua ama kutokujua lakini mwisho wa siku kimemuumiza mwenzio badala ya kuendela kuonyesha kuwa upo sahihi kubali tu umekosea. Na kama unadhani upo sahihi tafuta muda mwingine wote mkiwa na furaha uzungumze naye. Sasa unaona mwenzako kashakasirika pengine na kauli yako kali uliyoitoa badala ya kukubali umekosea unaanza kauli zile za kuudhi ‘Kama unaona nimekuudhi basi samahani’ Kha! sasa si umemuudhi na ndiyo maana kakasirika kwanini tu usisema ‘samahani nimekukasirisha’ au wakati mwingine sasa mtu naye anaanza kuleta visa vilivyotokea zamani kuonyesha pia na yeye alishawahi kukukosewa. Huo siyo muda wake jamani kama ulikosewa huko zamani hayo si ni ya zamani? Tunazungumza ulichokosea leo. Cha muhimu kubali umekosa hata kama unajua upo sahihi muda utapatikana wa wewe kuzungumza hoja yako lakini wote mkiwa mmetulia.
D
Jifunze kuwa msikivu. Wakati mwingine anachohitaji mwenzio ni kusikilizwa. Mpe nafasi ya kuzungumza na wewe jipe nafasi ya kusikiliza. Siyo lazima uhoji kila jambo analozungumza mpenzi wako. Kumbuka kama unavyopenda kusikilizwa wewe basi kila mtu naye anapenda kusikikilizwa hivyo hivyo. Siyo hata mtu hajamaliza kuzungumza alichotaka kusema ushadakia. Jamani kama unataka kuongea si utafute na wewe muda wote uzungumze? Elewa kwamba siyo kila muda unapaswa kuzungumza muda mwingine unatakiwa kusikiliza tu na kuelewa.
E
Usimfiche mpenzi wako kitu chochote. Hata kama kitu hicho kilikutokea ama ulikifanya zamani wakati haupo naye lakini ilimradi unajua kabisa kinaweza kuleta shinda katika mahusiano yenu mwambie mapema ili kuzuia tafrani. Ni vizuri umwambie wewe mwenyewe kuliko aje kusikia kwa mtu mwingine huko barabarani. Kumbuka ukweli pekee ndiyo utakao kuweka huru. Ukidanganya chochote katika mahusiano yako utaishi maisha yasiyokuwa na furaha huku ukiwaza itakuwaje siku akigundua. Utajikuta unakuwa mtumwa katika maisha yako mwenyewe na kamwe hautakuwa na furaha ya kudumu.