SIKU moja nilikuwa nimekaa kijiweni na marafiki zangu, mara akatokea kijana mmoja na kuanzisha mada iliyohusu jinsi mapenzi ya siri yalivyo matamu.
Wakati anaanzisha mada hiyo ilikuwa vigumu kumuelewa lakini baadaye nikagundua amepata demu ila penzi lao ni la siri kwani hataki watu wengine wajue. Nilishangaa sana!
Nikamuuliza sababu za yeye kukubali kuingia kwenye penzi la siri, akadai yeye mwenye ana videmu viwili ambavyo anatoka navyo kwa siri sana hivyo mazingira hayo yatamfanya awe salama zaidi.
Maelezo ya kijana huyo yalinifanya nijifunze kitu ambacho nimeona si vibaya nikawamegea na nyie.
Ukijaribu kufuatilia utagundua kuna watu wengi sana wako katika mapenzi ya siri kutokana na sababu wanazozijua wenyewe. Pia ukiendelea kuchunguza utabaini wengi walio katika mapenzi ya siri ni watu na ndoa zao.
Unakuta mwanamke kaolewa, vidole vyake vimepambwa na pete za gharama za uchumba na ndoa lakini kutokana na tamaa zake anatafuta ‘kidumu’, yaani mwanaume mwingine nje ya ndoa na kuomba iwe siri kwani bado anampenda mumewe.
Si wanawake tu, wanaume nao baadhi yao walio katika ndoa wametafuta nyumba ndogo. Wanahudumia kila kitu, wanapewa huduma za kimahaba pale wanapohitaji lakini kwa siri sana ili wake zao wasijue.
Lakini mbaya zaidi ili ujue kwamba mapenzi ya sasa ni sarakasi tupu, wapo wake za watu wanaoanzisha uhusiano na waume za watu, vivyo hivyo waume za watu wanaoanzisha uhusiano na wake za watu.
Wanaofanya hivyo, wala hawaoni kwamba ni hatari. Wanakuwa na amani kutokana na makubaliano yao kwamba mapenzi yao yawe ya siri.
Wengi wamefanikiwa katika hilo lakini naomba niseme tu kwamba, uhusiano wa sampuli hiyo ni sawa na kutembea na bomu mfukoni, wakati wowote litalipuka na utajuta kuzaliwa.
Nasema utajuta kwa kuwa, hebu vuta picha wewe ni mume wa mtu halafu unafumaniwa na mke wa mtu na mwenye mke kwa kusaidiana na wapambe wake wanakutembeza mtupu mtaani, utajisikiaje?
Ni afadhali hata ukafumaniwa na kabinti (siyo poa pia) lakini mke wa mwanaume mwenzako! Hivi roho itakusutaje? Una kila sababu ya kujiangalia upya kama una katabia hako.
Ifike wakati uridhike na kile unachokipata kutoka kwa mwenza wako. Tamaa zako za kijinga zitakufikisha pabaya na kujikuta unauchukia ulimwengu.
Lakini leo nataka niwazungumzie kwa kifupi sana hawa ambao hawako kwenye ndoa lakini wanaingia kwenye uhusiano wa siri huku sababu zinazotolewa zikiwa hazina mashiko.
Wataalamu wa masuala ya mapenzi wanaeleza kuwa, penye penzi la kweli hakuna usiri. Mtaficha weee lakini mwisho wa siku watu watajua ila mkiona mmefanikiwa kuwafanya watu wasijue kwamba nyie ni wapenzi basi mnadanganyana, hapo hakuna mapenzi ya kweli.
Lakini wataalamu hao wa mapenzi wanasema, kama utakubali kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi wa siri, tarajia mambo mawili makubwa kukutokea!
Kusalitiwa
Staili ya ‘penzi letu liwe la siri’ hutumiwa sana na wale ambao wametawaliwa na tamaa za kijinga, wasioridhika na mpenzi mmoja. Matokeo yake sasa kila anayemtamani anamchomekea lakini anaomba penzi liwe la siri ili wengine wasijue.
Ndiyo maana nikasema, mpenzi wako akikuambia uhusiano wenu uwe wa siri na ukakubali iwe hivyo, kaa mkao wa kusalitiwa.
Kubambikiwa
Kama wewe ni mwanaume na ukakubali kuwa na uhusiano na msichana kwa siri, ni rahisi sana kubambikiwa hasa linapokuja suala la mimba.
Mpenzi wako anaweza kutembea na mwanaume mwingine kwa siri na akapewa ujauzito lakini kwa kuwa unajua kwamba wewe ndiye ambaye uko naye, huwezi kuikataa, utasema ni yako kumbe umeingizwa chaka! Umenisoma?