Sunday, March 18, 2018

UNAYAJUA MAUMIVU YA MAPENZI? SOMA HAPA !!!

HAKUNA mwenye moyo ambaye anafurahishwa na maumivu katika mapenzi. Hapa nazungumzia usaliti, unyanyasaji, masimango na mengine mengi katika uhusiano wa kimapenzi.
Wapo watu ambao ni wa kwanza kuwaumiza wenzao lakini wao wakiumizwa ni matatizo tupu! Wanajihisi kama wao pekee ndiyo wenye moyo wa kuumia lakini wenzao hawapati maumivu. Hivi hii inaingia akilini kweli?
Marafiki zangu, lazima tufahamu kwamba mioyo yote ina nyama. Kuna mambo mengi ambayo mpenzi akifanyiwa na mwenzake lazima ataumia sana. Ingawa kuna mengine yanafichwa au kupasishwa kama sahihi, lakini ukweli unabaki pale pale kwamba yanaumiza.

Kikubwa ambacho unatakiwa kufahamu ni kwamba maumivu hayo yapo sawa kwa kila mmoja. Haijalishi jinsia, umri, kabila wala dini, maumivu ya mapenzi yote yanafanana. Kufanana huko kunasababishwa na mioyo yote kuwa na nyama!
Kwa sababu mioyo yote ina nyama basi unatakiwa kufahamu kwamba, jinsi unavyoumia wewe moyoni mwako, ndivyo mpenzi wako anavyoumia ikiwa utamfanyia makosa kama ambayo unamfanyia wewe.
 
UMEWAHI KUWAZA KUHUSU KUSALITIWA?
Unajua kabisa una mpenzi, tena inawezekana wakati mwingine mmeshawahi kuzungumza juu ya kuishi pamoja, lakini bila haya wala aibu, unamsaliti! Kwa nini unafanya hivyo? Kama umeona hana thamani tena kwako, kwa nini unazidi kumpotezea muda?
Unafikiri anafurahia sana wewe kuwa na kimada mwingine huko uchochoroni au unadhani atafurahia siku akijua kuwa una mtoto umezaa nje ya ndoa yako? Nafsi yako yenyewe inakusuta, inajua ni kiasi gani unamkosea mpenzi wako lakini unajifanya kichwa ngumu na kuendelea na uchafu wako. Kwa nini hutaki kubadilika?
Hebu jitoe katika nafasi yako, kisha mfanye mpenzi wako ndiyo wewe, halafu fikiria kama yeye ndiyo angekuwa anakusaliti, ungejikiaje? Lazima utaumia! Sasa kama utaumia kwa nini unaendelea kumfanya mwenzako akose raha?
Lazima uwe na moyo wa huruma, akili yako ifanye kazi ipasavyo na kugundua makosa unayoyafanya kisha kufanya mabadiliko ya haraka. Amini jinsi utakavyoumia kwa kufanyiwa mabaya na mwenzako ndivyo mpenzio anavyoumia kwa mabaya unayoyafanya.
Wengi wamekuwa wakiwasaliti wapenzi wao wakiwa hawafikirii siku ya wao kufanyiwa hivyo itakavyokuwa. Hebu vuta picha, unakwenda nyumbani kwa mpenzi wako, unagonga mlango haufunguliwi!

Baadaye unahisi kama ndani kuna watu, hilo linaingia akilini mwako baada ya kuona viatu vya mpenzi wako pamoja na viatu vingine vya jinsia tofauti ya mpenzi wako.
Unaamua kusukuma mlango na kuingia ndani, hamadi! Unakuta mpenzio akiwa kitandani na mtu mwingine. Utajisikiaje? Jiweke katika nafasi hiyo. Naamini kabisa ni lazima utajisikia vibaya sana, sasa kama ndivyo, kwa nini wewe unamsaliti?
Mapenzi ya kweli hayaambatani na usaliti. Penzi la kweli lina uaminifu wa dhati, kuchukuliana, kupendana, kusaidiana, ukarimu, huruma na mengine mengi ambayo huyafanya mapenzi yazidi kuwa imara kila siku.
 
USIJIFIKIRIE MWENYEWE...
Vipengele vilivyopita vinafafanua hili kwa undani, lakini kwa kuongezea ni kwamba huna sababu ya kujiwazia wewe mwenyewe! Kujiona wewe pekee ndiye mwenye haki ya kuwa salama katika penzi lako.
Chunga nafsi yako lakini wakati huo huo ukiangalia kwa jicho la tatu, nafsi ya mwenzako. Kila mmoja anaumia anapohisi kusalitiwa, hivi unafikiri ni nani anayependa kushea mapenzi? Hakuna.
Utakuta mwingine simu ya mpenzi wake ikiita anakuwa wa kwanza kuichukua na kutaka kupokea au kusoma sms, lakini subiri sasa simu yake iite; Anakuwa mkali zaidi ya mbogo! Acha kujifikiria peke yako.
 
KIPO CHA KUFANYA!
Siamini kama kuna ambacho sijaandika katika vipengele vyote vilivyopita, lakini hapa nakusisitizia kufanya mabadiliko ya haraka ili mwisho wa siku uweze kuishi maisha mapya, mazuri, yenye mapenzi ya kweli huku moyo wako ukiwa huru.
Hutakuwa na maumivu moyoni mwako, maana utakuwa unamtendea haki mpenzi wako. Lakini kama ukiendelea kumsaliti, ujue wazi kwamba utakuwa unajizidishia maumivu katika moyo wako.
Huo ndiyo ukweli!