Wednesday, March 21, 2018

Madhara ma-3 ya mwanamke kushobokea penzi la pesa!

Mpenzi msomaji wangu, ni wiki nyingine tulivu kabisa tunakutana kupitia ukurasa huu namba moja kwa kuandika makala nzuri za mahusiano.Ni matumaini yangu kwamba umzima na unaendelea vyema na mchakamchaka wa maisha.
Wiki iliyopita utakumbuka nilizungumzia dalili 5 za mwanamke mwenye mchepuko. Ni makala iliyoonekana kuwagusa wanaume wengi huku baadhi wakidai kuwa, wapenzi wao wanazo lakini wanashindwa kuwaacha kwa kuwa wanawapenda sana.
Sikiliza ndugu yangu, maisha yako ni vile unavyotaka yawe. Maisha ya furaha au ya huzuni unaamua wewe, sasa kama umebaini mpenzi wako hajatulia na bado unashindwa kufanya maamuzi sahihi, hiyo ni shauri yako.
Mimi nimeshasema, ukiona dalili zile tano, ujue unasalitiwa na unachotakiwa kufanya ni kumuacha huyo mpenzi ambaye hajatulia. Ukiona ni sawa kuendelea naye kwa kuwa unampenda, mimi sikulazimishi umuache. Sawa jamani?
Baada ya kugusia kidogo mada hiyo ya wiki iliyopita, nirudi sasa kwenye mada ya wiki hii kuhusu madhara ya kushobokea penzi la pesa.
Mapenzi ni sehemu ya maisha yetu na kwa hakika maisha yetu hayawezi kukamilika bila kuwepo mapenzi. Ninapozungumza juu ya mapenzi namaanisha yale yanayotoka moyoni mwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine.
Mapenzi ni nguzo ya maisha yetu, kama ukifanikiwa kumpata mpenzi ambaye atakupenda na wewe ukampenda ni wazi kuwa maisha yako yatakuwa yenye furaha!
Wakati mwingine unaweza ukapendwa na mpenzi ambaye hujampenda, unadhani kuna ulazima wa wewe kulazimisha kumpenda?
Moyo wako umeshazungumza na wewe, umekuweka wazi kuwa hauna mapenzi ya dhati kwa mtu huyo, kwa nini ujilazimishe eti kwa sababu umeona mtu huyo ana uwezo kifedha?
Kama ulikuwa hujui, ukilazimisha kumpenda mtu kwa kuwa ana mali nyingi, pesa kwake siyo tatizo, ipo siku utajuta hasa pale ambapo utabaini kuwa, huna mapenzi ya dhati na mtu huyo bali tamaa yako ya pesa ndiyo iliyokuingiza huko.
Tatizo hili mara nyingi huwa kwa wanawake! Anatongozwa na mwanaume, mwanaume huyo anajinasibu kwa uwezo wake na jinsi alivyompenda kwa dhati. LaKini kwa bahati mbaya unaweza kukuta msichana huyo wala hana hata chembe ya penzi kwa mwanaume husika.
Lakini kwa tamaa yake, anakubali akijipa matumaini kuwa, atajifunza kupenda akiwa ndani ya penzi. Nani kakudanganya kuwa unaweza kuingia kwenye uhusiano na mtu usiyempenda kisha ukajifunza kumpenda mkiwa ni wapenzi?
Hili ni jambo ambalo haliwezekani na wengi ambao waliingia kwenye uhusiano kwa sababu ya pesa au mali, leo hii ndiyo wanaoongoza kwa kuachika na kusaliti.
Ndiyo! Ni lazima hayo yatokee kwa sababu, kama humpendi bali umependa pesa zake, ukiwa naye ndani ya ndoa lazima utatafuta yule unayempenda kwa dhati na matokeo yake utaanza kuchepuka.
Ukishaanza katabia hako, kwanza utaleta magonjwa ndani ya ndoa, pili kuna siku utabainika na kuambulia talaka kama siyo kipigo lakini tatu utaonekana ni mwanamke ambaye hujatulia.
Sasa kwa nini hayo yakukute? Kwa mwanamke anayejitambua hawezi kuingia kwenye uhusiano na mtu ambaye hampendi. Atafanya mawasiliano na moyo wake kwanza, ukikubali kuwa na mtu huyo ndiyo ataingia lakini moyo ukisita hata kama ameona mwanaume aliyemtokea ana fedha na mali nyingi, atamuacha apite.

Hii yote ni kwa sababu, penzi la dhati ndilo linaloweza kukupa furaha maishani mwako. Ukimpenda mtu eti kisa mali zake, huwezi kuipata ile furaha uliyoitarajia hivyo ni vizuri ukawa makini katika hilo.
v