Wednesday, January 3, 2018

Mambo 5 Yanayoleta Uadui Kwa Wapenzi !

Rafiki, bila shaka ipo wazi kwamba kila mmoja anapenda kuwa na mpenzi ambaye mbali na kumpenda kwa moyo wake wote, atapenda kumfanya awe kama ndugu, rafiki au zaidi ya hapo. Atakayekuwa tulizo la moyo, kivuli kwenye jua kali, maji jangwani na tiba kwenye maradhi.

Hakuna anayeweza kuukabidhi moyo wake kwa mtu ambaye anajua fika kwamba atamtesa, atamnyanyasa, kumsababishia maumivu ya moyo, kuwa kero kwenye maisha yake na ‘kum-treat’ kama adui yake.

Mapenzi ni sanaa kama zilivyo sanaa nyingine. Kwa mfano, ili kumudu kupiga gitaa au kinanda na kupata muziki mzuri, ni lazima ujifunze. Kwenye mapenzi ni hivyohivyo, ili kuishi vizuri na mpenzi wako ni lazima ujifunze. Usichoke kujifunza kila kukicha ili kuwa na uhusiano imara na ndoa inayoweza kudumu, jifunze kupenda na kumuenzi umpendaye kwa moyo wako wote.

Labda nikuulize rafiki yangu, wewe ulijifunzia wapi mapenzi? Shuleni, nyumbani, chuoni, mitaani au mtandaoni? Yawezekana ukatafsiri mapenzi kwa maana ya tendo la ndoa lakini hapa simaanishi hivyo, nazungumzia sanaa nzima ya mapenzi katika tafsiri pana.

Ukweli ambao unashangaza, watu wengi wana uelewa mdogo juu ya suala zima la maisha ya kimapenzi, jambo ambalo linasababisha waishi kimazoea na kushindwa kufuata misingi halisi ya jambo hilo nyeti katika maisha.

Matokeo yake, watu ambao awali wakati wanaanzisha uhusiano wa kimapenzi walikuwa wanapendana na kugandana kama ruba, huishia kuwa maadui na kuvunja uhusiano wao kwa majuto mengi. Yaani mtu ambaye awali alikuwa kipenzi cha roho yako, anabadilika na kuwa mwiba mkali maishani mwako.

NINI HUMFANYA MPENZI AWE ADUI?

Kwa kawaida, mnapoanzisha uhusiano wa kimapenzi kila mmoja humueleza au kumuonesha mwenzake nini anapenda na kipi hakimfurahishi. Kwa kuwa mapenzi ni suala la hiyari, mwenzio anapokukabidhi moyo wake anategemea kuwa utayafanya yale yanayomfurahisha na kuepuka yale yanayomuudhi kwa kadiri uwezavyo. Wataalam wa mapenzi wana msemo mmoja kwamba ‘penzi la kweli humsukuma mtu kumfurahisha mpenzi wake kwa kadiri ya uwezo wake na kamwe halitafuti visingizio’.

Usitafute visingizio linapokuja suala la kumfurahisha mwenzio. Yafuatayo ni baadhi ya mambo ambayo yanaweza kumgeuza mpenzi wako akawa adui yako.

1.UKISHINDWA KUMSIKILIZA

Mapenzi ni kusikilizana kwa kila jambo, hakuna nguzo muhimu kama kukubali kuupokea udhaifu wa mwenzako. Jenga mazoea ya kumsikiliza mpenzi wako kwa staha! Hata kama amekukwaza (lazima itatokea tu kwani yeye siyo malaika), tafuta namna nzuri ya kufikisha hisia zako kwake.

Kabla ya kumsikiliza usikimbilie kumhukumu, kumsimanga, kumvunja moyo au kutoa kashfa ambazo zitamfanya asononeke ndani ya moyo wake kwani vitu hivyo vikizidi, hupunguza hisia za upendo na chuki huanza kujengeka taratibu.

2. MAUDHI YA MARA KWA MARA

Wachambuzi wa masuala ya mapenzi, wanaeleza kwamba miongoni mwa sumu ambazo zinaweza kumgeuza mwenzi wako na kuwa adui yako ni kitendo cha kumfanyia maudhi yanayojirudia.

Kama unataka kuishi kwenye uhusiano wenye amani, epuka maudhi ya mara kwa mara kwa mwenzako. Endapo ameshakwambia kwamba jambo fulani halipendi, msikilize na muoneshe kwa vitendo kwamba umebadilika.

3. KUFOKEANA MBELE ZA WATU

Yawezekana amekuudhi kiasi kwamba umeshindwa kuzidhibiti hasira zako, matokeo yake unaanza kumpandishia au kumfokea mbele za marafiki zake, ndugu au watoto. Jambo hili hujenga chuki kali ndani ya moyo wa anayetendewa na taratibu ataanza kukutoa thamani.

Hata kama umechukia kiasi gani, kamwe usimfokee mwenzako mbele za watu, tafuta muda ambao utakuwa umetulia, zungumza naye kwa upole na bila shaka mtafikia muafaka wa kilichokuwa kimekukasirisha.

4. KUSHINDWA KUHESHIMU NDUGU ZAKE

Familia zetu za Kiafrika, tuna kawaida ya kutembeleana mara kwa mara, yaani kama ni mume, ndugu wa mke watakuja nyumbani kwenu na kama ni mke, ndugu wa mume watakuja nyumbani kwenu.
Hakuna jambo baya kama kuonesha chuki kwa ndugu wa mwenzako, hii itamfanya mwenzako aamini kwamba mapenzi yako kwake ni ya msimu. Taratibu ataanza kukushusha thamani.

5. KUKOSA UAMINIFU

Jambo kubwa ambalo ndiyo mhimili wa uhusiano wowote wa kimapenzi ni uaminifu kwa mwenzi wako. Mapenzi ya kweli yanajengwa na uaminifu, kamwe usithubutu kuuchezea kamari moyo wa mwenzako. Yaani yeye anakupenda na kukupa heshima zote unazostahili lakini nyuma ya pazia, unachepuka na mwingine.

Hata kama alikuwa anakupenda vipi, akigundua upendo utabadilika na kuwa chuki kali ndani ya moyo wake ambayo itadumu kwenye moyo wake. Jitahidi kumfanyia mambo mazuri na kamwe usiuumize moyo wake.