Sunday, January 21, 2018

MAHUSIANO BAADA YA USALITI.


Baada ya affair kutokea au kugundulika huwa ni wakati mgumu kwa wanandoa; jambo la msingi ni kwamba kuaminiana kulikoyeyuka huweza kurudi hasa baada ya hasira kwisha na wanandoa kuanza kuwa karibu kihisia tena.
Hii hutokea tu na pale tu kama wahusika wameelezana na kufahamu sababu za kwa nini affair ilitokea.
Ukweli ni kwamba kuelezea sababu za kwa nini affair ilitokea ni moja ya jambo gumu sana na pia ni moja ya jambo muhimu sana katika kuiponya ndoa.
Ni muhimu kujua sababu za affair kwa kuwa kama wewe ni uliyesalitiwa na mwenzako utatakiwa kujifunza kwa mapana yote kwa nini mwenzako alichepuka (affair) ili kuweza kurudisha ukaribu wa kimapenzi na kuaminiana upya.
Kama wewe ndiye umesaliti ni vizuri kuelezea sababu za kuchepuka kwako kwa sababu ndicho mwenzako anapenda kufahamu.
Kujua sababu za affair ni kuchambua au kuweka wazi sababu zilizofanya mwingine achepuke.
Ili kufahamu vizuri maana ya kwa nini affair ilitokea hebu tujaribu kuweka suala la affair katika ndoa kama vile nyumba inavyoingiliwa na majambazi usiku.

Baada ya nyumba kuvunjwa ni muhimu kuchunguza nini kilifanya majambazi kuvunja na kuingia kuiba kirahisi, ni mianya ipi ilisababisha hao wezi kuvunja na kuingia kirahisi?
Je, tatizo ni majirani hatari?
Na je, ulichukua hatua gani kujilinda na hao majirani ambao wamesaidia kuwapa majambazi data au siri na namna ya kuvunja na kuingia katika nyumba yako?
Je, uliwaona watu wageni ambao walikuwa wanapita karibu na nyumba na hukutilia maanani na ukaona ni jambo la kawaida?
Je, nyumba yako haikuwa na milango ya uhakika?

Kuingiliwa na majambazi na kuibiwa haina maana kwamba unawajibika na tabia mbaya za wale majambazi.
Hata hivyo ukihamia nyumba nyingine utajisikia secured kama utafahamu sababu zilizofanya majambazi kupata mwanya wa kuvunja na kuingia kukuibia nyumba yako ya kwanza.
Hutakuwa na uhakika wa usalama wako kuibiwa na majambazi kama hutafahamu sababu zilizofanya uibiwe mara ya kwanza.
Trust na usalama wa kuwa karibu kimapenzi katika ndoa umeharibiwa na mwenzako ambaye amekusaliti, kama majambazi walivyoingia na kuvunja nyumba na kuiba, hutakuwa salama hadi ujue sababu zilizochangia.
Au inawezekana mmoja wenu alikuwa na urafiki na mtu wa nje ambaye alikuwa hana heshima na ndoa yenu.
Pia inawezekana kulikuwa na dalili za mwenzako kutoka nje na wewe ukapuuzia. Inawezekana hakukuwa na ukaribu wa kimapenzi kati yenu na hiyo ikatoa mwanya kwa yeye kuvutiwa kihisia na mtu wa nje.
Inawezekana kuzozana kwenu kila siku kumefanya muwe mbali kimapenzi na kihisia hivyo kutoa mwanya kwa mwingine kutoka nje.
Inawezekana mmoja alikuwa hamheshimu mwenzake na alipopata anayemheshimu nje akaishia kuchepuka.
Inawezekana kulikuwa na ukame wa tendo la ndoa ndani ya ndoa yenu na mwingine akajikuta anapenda kutuliza kiu nje.
Au inawezekana ni shetani tu.............................
Ukishajua sababu basi inakuwa rahisi kubadilisha mambo na si wanandoa wote huwa tayari kukubaliana na hizi changamoto.