Sentensi 3 Zinazotajwa Kawaida, Ambazo Mwanamke Hapaswi Kabisa Kumwambia Mmewe/Mchumba
Ulimi ni kiungo muhimu sana kwenye maisha ya binadamu. Neno moja linaweza kujenga au kubomoa ukuta mkubwa wa ndoa uliojengwa kwa gharama kubwa ya uvumilivu, uaminifu na upendo.
Hivyo, ni jambo muhimu sana kukumbushana japo kwa machache baadhi ya sentensi zinazotumika mara kwa mara na kuonekana kuwa za kawaida, lakini zinaweza kuwa chanzo cha kuvunja ndoa au kuvuruga uhusiano uliostawishwa kwa gharama kubwa.
Leo nitagusia sentensi tatu za kawaida kabisa ambazo hutumiwa na baadhi ya wanawake bila kufahamu kuwa zinaweza kuwa chanzo kikuu cha kuutafuna uhusiano wao.
- “Mama Yangu Alinionya Kuwa Utanifanyia Hivi.”…
Sentensi hii inaweza kumfanya mmeo kuwaza mengi sana kuliko ulivyomaanisha wewe pale unapotaka kumkosoa kwa alichokifanya. Kwanza atagundua kuwa una watu wengi nyuma yako ambao wanakusaidia kumfikiria ‘hasi’.
Kibaya zaidi unapomuweka kwenye kundi hilo mama yako ambaye yeye anamheshimu sana. Hii linaaweza kupelekea mchumba au mme wako kutokumuamini mama yako na kuanza kumuona kama adui wa uhusiano wenu. Unadhani mama yako akiwashauri jambo atalichukuliaje? Hata kama ni zuri.
- “Unafikra Kama Za Baba Yako” (Unapomkosoa)
Bila shaka unafahamu ni kiasi gani wanaume huwaheshimu sana na kuwaamini sana baba zao ambao wamewashauri mengi hadi walipofika hapo. Hata kama huwa anakueleza baadhi ya fikra au mawazo ya baba yake asiyokubaliana nayo, usidhubutu kabisa kumtolea mfano kumuonesha kuwa na wewe unamchukulia hivyo mzazi wake.
Kukosoana ni suala zuri katika maisha ili kurekebishana lakini angalia njia nzuri ya kupinga hoja ya mwenzi wako, kwa ustaarabu kuepuka kumkera.
- “Hivi Lini Utapata Kazi Mpya..?”
Swali hili sio baya lakini kwa jinsi lilivyoulizwa lina kila dalili za kuleta shida sana kwenye fikra za mumeo/mchumba wako. Kwanza atajua ni kiasi gani unafikiria vibaya kuhusu maisha yenu hasa kiuchumi.. Ni bora kumwambia, “Mume wangu ninakuombea sana upate kazi mpya.” Ni ujumbe uleule lakini jinsi ulivyofikishwa unatofautiana sana.