SABABU MBOVU ZA KUINGIA KATIKA MAHUSIANO/NDOA
(Fahamu kwanini wengi hujuta baada ta muda mfupi kwenye ndoa)
Watu wengi tumewaona kwenye ndoa wakiishi katika hali tofauti za maisha, wako wenye fedha na wasionazo, wako wenye furaha na wasionayo. Yote hii huweza kuchangiwa na sababu nyingi ikiwemo wanandoa hawa kujikuta wanaingia katika ndoa wakisukumwa na sababu zilizo mbovu na zisizo na msingi.
Ziko sababu njema na nzuri za ndoa zinazoongelewa sana na wengi maeneo mbalimbali. Mimi nimejaribu kuzitafuta zile sababu zisizo nzuri ambazo wengine pasipokuwa makini wamezishikilia na kusiruhusu sababu hizi ziwasindikize katika ndoa na hivyo kujikuta wenajuta na kulia katika muda mwingi wa maisha baada ya mahusiano hayo.
Hii pia ni sababu ya ukweli kwamba siku hizi idadi ya ndoa zinazovunjika ni kubwa sana kuliko awali. Hali ya kiwango cha kudhamiria (commitment) kwa wanandoa ni kidogo sana na hivyo kushusha uthamani wa ndoa zenyewe.
Sababu hizi zitakuwezesha kuubadili mtazamo ulionao juu ya ndoa na kukupelekea kubadili namna unavyo sema au kuwaza au kutenda kuhusiana na suala zima la ndoa na mahusiano.
SABABU MBOVU
- Kuingia katika ndoa/mahusiano kwa lengo la kusaidiwa au kuongeza kiwango cha kiuchumi ulicho nacho.
Katika penzi la namna hii hakuna mguso au muunganiko wa kuhisia (intimacy) baina ya wapenzi, bali kinachowaunganisha pekee ni kile kilicho mfukoni au vile vinavyoshikika na kuonekana tu. Athari za penzi la aina hii lina fungua milango mingi kwa wahusika kutokuwa waaminifu na hata kujihusisha na mapenzi nje ya mahusiano yao.
- Hofu ya umri kupita na kuzeeka
Wako wengine ambao kwasababu wanakiu sana ya kupata watoto na wameogopeshwa sana habari kwamba wana weza wasipate watoto kwa sababu ya umri wao, basi watacheka na kaka yeyote yule ilimradi tu waolewe au wazae naye. Wengine wajinsi hii wamejuta sana baada ya kujikuta kuwa waliyezaa naye hakuwa BABA bali mwanaume tu, tena kirukanjia tu na kwahiyo wanawake hawa wameishia kulea mtoto au watoto wao wenyewe pasipo mzazi wa pili (single parenting), jambo ambalo kwa kiasi kikubwa linawaathiri watoto wengi. Kwa wale wanaokimbilia kuolewa ili wakazae watoto, kukumbuka kuwa hata huko kwenye ndoa kuna waliokosa watoto.
- Kuingia kwenye ndoa sababu ya mimba au mtoto aliyepatikana kabla ndoa
- Kulazimika kuingia kwenye ndoa au mahusiano ya kudumu kwasababu ya upweke, (Loneliness).
- Kuolewa au kuoa kwasababu ya shinikizo kutoka kwa wazazi, ndugu au marafiki
- Kuamua kuoa au kuolewa ili kupata uhuru.
MATOKEO YA KUINGIA KATIKA NDOA KWA SABABU MBOVU
Lengo la kuingia kwenye ndoa, liwe zuri au liwe baya ndilo litakalotegemeza aina ya maisha yenu katika ndoa hiyo kuwa ya furaha au ya machungu. Baada tu ya kuoana na huyo mtu wako kwa sababu zisizo za msingi, siku, miezi au miaka siyo mingi utaanza kuchoka na kutamani kutoka nje ya hiyo ndoa kwa maana baina yenu hakuna muunganiko wa ndani (emotional attachment) baina ya wanandoa wawili. Na mara nyingi hali hii hupelekea msongo wa mawazo (stress), mfadhaiko wa moyo na kukosa furaha ndani ya ndoa. Na matokeo ya hali hii kumfanya mwanandoa mmoja au wote wawili kuanza kutafuta kutoshelezwa na kuliwazwa nje ya ndoa na hapa vinazaliwa vitu vingine kama uzinzi, kutengana, talaka au magomvi na mifarakano isiyoisha.
Kwanini ndoa na mahusiano mengi hushindwa?
Kwa sababu ya kukosa maarifa.
Wanandoa wengi hawajui nini wafanye, nini waelewe ili kufanya ndoa yao zifanikiwe. Thamani ya ndoa na jinsi ndoa inavyochukuliwa sikuhizi ni tofauti sana na nyakati za wazazi wetu, na hii imewafanya wengine kujikuta wako wenye ndoa kwasababu mbovu na hivyo ndoa nyingi kuvunjika au kuyumba baada ya muda mfupi tu. Vitu kama kudhamiria, heshima na uaminifu sio vya maana tena siku hizi, sababu watu wanaogopa kuonekana wazamani na washamba.
Mtazamo wa ulimengu juu ya ndoa umeharibiwa na magazeti, luninga na vitabu mbali mbali. Siku hizi kuishi bila ndoa ni kitu cha kawaida, kuwa na mpenzi nje ya ndoa sio kitu cha ajabu tena, mapenzi nje ya ndoa sio ya kushangaza hata kidogo. Kinyume chake ukionekana kuyashangaa haya, jamii itakushangaa wewe kwa jinsi ulivyo nyuma ya wakati. Mambo yamebadilika sana, zamani binti akikutwa bikira wakati anaolewa ilikuwa sifa kwake na familia nzima, siku hizi binti akikutwa bikira atachekwa, na watu kumshangaa wakihisi ana matatizo fulani. Hali kadhalika kwa kijana wa kiume aliyejitunza. Kwa bahati mbaya sana tunaishi katika jamii ya ajabu isiyoamini katika kujitoa kwa kweli na kudhamiria katika mahusiano. Jamii isiyoamini katika uaminifu, na ndiyo maana magomvi mengi hutokea pale simu ya mmoja inapoguswa. Kuwindana na kuchunguzana kumekuwa kawaida, maadili sio jambo la kuzingatiwa tena. Wanandoa wengi ni wale wenye majeraha ya moyoni na walio umizwa, kwa hiyo hutoka nje ya ndoa zao wakitafuta mwingine aliyeumizwa kama wao ili waliwazane.
Kwa haraka tuangalie sababu za msingi zinazoweza kukufanya uingie katika ndoa na usijute.
- Ndoa ni mpango wa Mungu kwa mwanamke na mwanaume kuwa pamoja
- Ni nafasi ya wawili hawa kuonyeshana mapenzi yao
- Ni nafasi ya kutimiziana mahitaji ya mwili kupitia tendo la ndoa kwa muda sahihi, na kwa mtu sahihi, maadili yakizigatiwa.
- Hamu na kiu ya kutengeneza familia yenu.
- Kutimiza kiu ya kuwa pamoja kwa umoja (companionship)
- Nia au kusudi la kushiriki vyote kwa pamoja . Kufanya kutenda kwa pamoja ili kutimiza mahitaji yetu wote.
navyo kwa maendeleo ya familia.
- Kuchangiana katika makuzi yenu ya ujumla, makuzi ya kimwili, kiroho, kihisia n.k