Mchungaji wa Nigeria anayefahamika kama mchungaji Augustine Mendie, mkazi wa Eket Akwa Ibom, amejikuta katika matatizo makubwa baada ya kulazimishwa kuoa mwili wa marehemu ambaye alikuwa mwimba kwaya wa kanisa hilo aliyempa ujauzito.
Kwa mujibu wa Daily Post, mchungaji huyo ambaye ana mke na watoto alimpa ujauzito mwimbaji huyo na baada ya kuelezwa alimshauri kuitoa ili mambo yasiharibike kanisani na kwenye jamii. Baada ya ushawishi wa muda, msichana huyo alikubali kutoa mimba kwa fedha alizopewa na mchungaji Mendie.
Hata hivyo, zoezi la kutoa mimba halikwenda vizuri na kupelekea msichana huyo kupoteza maisha. Kwa bahati nzuri msichana huyo aliwahi kumsimulia rafiki yake wa karibu kuhusu kinachoendelea kati yake na mchungai Mendie akimtaka aitunze siri hiyo. Lakini baada ya kumuona rafiki yake amepoteza maisha aliijuza familia yake ukweli wote na ndipo mchungaji alipotiwa mikononi mwa jamii.
Baada ya kuhojiwa na uongozi wa jamii hiyo alikana kuhusika lakini vitisho vya kutumia mizimu vilipelekea kukiri makosa yake.
Ndipo jamii hiyo ilipomlazimisha kuoa maiti ya msichana huyo ambaye alikuwa kiongozi wa kwaya katika kanisa lake, ili kukamilisha matakwa ya kimila ya jamii hiyo kabla hajakabidhiwa mikononi mwa polisi.
Vyanzo kutoka ndani ya kanisa hilo vilieleza kuwa mchungaji Mandie alikuwa na tabia ya kufanya uzinzi na baadhi ya waumini wake ikiwa ni pamoja na akina mama wenye ndoa.