Tuesday, November 21, 2017

Mahusiano: Mitandao chanzo cha wanawake kupenda mapenzi ya gizani


Uhusiano wa mapenzi una mambo mengi, na kuta nne za chumba ndizo zijuazo siri ya ndani ya wanandoa hasa katika suala la tendo la ndoa ambalo kwa hakika ni sehemu ya mhimili wa ‘ndoa’.
Ingawa tendo la ndoa hufanywa kwa usiri kati ya wanandoa kwani ni sehemu ya faragha, utafiti unaonesha kuwa idadi kubwa ya wanandoa hujikuta katika usiri mwingine ndani ya faragha yao wakishindwa hata kuonana wanapojamiiana huku mitandao ikitajwa kuwa sehemu ya sababu.
Utafiti uliofanywa na mtandao wa Weight Watchers nchini Uingereza ukijumuisha watu 2000, umebaini kuwa asilimia 27 ya wanawake wanaona aibu kushiriki na waume zao kwenye chumba chenye mwanga kwakuwa wanaona aibu na wanaona miili yao haivutii kutokana na kuona mitandaoni miili ya wanawake wengine hasa mastaa inavyovutia.
“Nikiangalia kwenye mitandao jinsi wanawake wengine walivyo na miili mizuri, hasa mastaa ambao wamezaa kama mimi lakini wameweza kujirudishia, ninakosa kujiamini nikiwa mtupu na mume wangu, naona kama sivutii kama wale,” alisema Sheiilar Gregam.
Utafiti huo ulibaini pia kuwa asilimia 75 ya wanawake hawaipendi miili yao ilivyo huku asilimia 60 wakikwepa hata kujiangalia kwenye kioo wanapokuwa watupu kutokana na kutojikubali.
Wakati upande wa wanawake ukidai hayo, hali ni tofauti kwa wanaume ambao wameonekana kuwa katika hali ya kujiamini zaidi, wengi wakionesha kutamani kushiriki na wake zao kwenye chumba chenye mwanga.
Hery Wambura, Mkazi wa Tegeta, Dar es Salaam ameiambia Dar24 kuwa ingawa tendo la ndoa limekuwa likionekana kama ni tendo la siri sana, kwa wanandoa linapaswa kufanywa kwa ufaragha na sio usiri.
“Mwanaume hupenda kumuona mkewe ambaye ni ua lake na pambo lake la ndani, na hii huongeza mapenzi zaidi kama watafiti wengine walivyowahi kusema kuwa wanandoa kulala bila nguo hudumisha mahusiano zaidi,” alisema Wambura ambaye ni mwanandoa na baba wa watoto wawili.
mahusiano
Wanawake wanapaswa kutambua kuwa hawatakiwi kukosa kujiamini kwa kile wanachokiona kwenye mitandao ya kijamii kwani wanawake wengi hasa mastaa hutumia ‘app’ za siku zinazohariri ngozi kuonekana yenye mvuto zaidi ya uhalisia.
Lakini pia, mazoezi wanayofanya wanawake hasa mastaa husaidia kuiweka miili yao kwenye hali na muonekano mzuri muda wote licha ya kuwa na umri mkubwa.
Jennifer Lopez akiwa na umri wa miaka 46
Jennifer Lopez akiwa na umri wa miaka 46
Mfano, mwanamuziki  Jenifer Lopez anaonekana kama mrembo mwenye miaka 25 hadi 30 hivi, lakini kiuhalisia ni mama wa miaka 46, tena ni mama wa watoto mapacha, Emme na Maximilian. Siri ni mazoezi na nidhamu ya mlo.
Mwanamke yeyote anaweza kushiriki mazoezi na kufuata nidhamu ya mlo ili kuwa na mwili anaoutaka. Wapo wataalam wengi wa mazoezi katika kila mji ambao wanaweza kumsaidia mwanamke au mwanaume kuwa na umbo analolihitaji.
Usikimbilie kutumia madawa ya kutengeneza muonekano fulani au kuondoa mafuta, tumbo na mengine. Dawa kuu na salama ni mazoezi na mlo.
Kwa lugha ya kigeni naweza kusema ‘workout, stay in shape’.