Thursday, November 23, 2017

Kwa Nini Mrembo Wako Anaweza ‘Kukusaliti’ Ingawa Anaonesha Ana Msimamo?

Makala hii naiandika nikimlenga mwanamme, hususan yule aliyepata bahati ya kupendwa na mwanawake mzuri na mrembo mwenye misimamo katika uhusiano, asiye mapepe na asiye na nia ya kufanya usaliti hata kidogo kwa kuwa wanaamini upendo haugawanyiki.
Ingawa watu wengi tunaamini kuwa wanawake ni viumbe ambao hudanganyika kirahisi kuingia kwenye uhusiano, tafiti zinaonesha kuwa mwanamke akipenda hupenda kwa milango yote ya fahamu.

Hata hivyo, zipo sababu ambazo zinaweza kumpelekea mwanamke mwenye msimamo kwako kuanza kutetereka na mwisho wa siku akajikuta ameangukia mikononi mwa mwanaume mwingine akilisaliti penzi lenu. Ingawa mapenzi sio mashindano, lakini nakushauri katika kutekeleza majukumu yako kwenye uhusiano wenu fikiria kama vile yupo mtu sehemu fulani anaweza kuwa mshindani wako ghafla na usipokuwa makini ataichukua nafasi yako kiulaini.
  1. Kupoteza umakini  
Mwanamke anapokuwa katika mapenzi anapenda umchukulie kwa umakini kama mtoto mdogo anaetambaa. Yaani kila anachokifanya wakati akiwa na wewe au anachofanya kwa ajili yako kisipite bila kuonesha hisia zako kuwa umekiona.
Kwa mfano, mpenzi wako anapoamua kukaa saloon masaa kadhaa akitengeneza kucha zake na kope zake kama maandalizi ya kukutana na wewe huwa anamaanisha kukufurahisha sana wewe. Moyo wake utafarijika sana endapo utamuona na kumsifia au kumpa ‘comments’ zako kwa ujumla.
Kama mpenzi wako kila anapojitahidi kujiremba au kujiweka sawa kwa ajili yako huwa unaona kawaida tu. Kwa kuwa mwanamke mzuri kufuatwa na wanaume ni kawaida, endapo kuna mwanaume katika mazingira aliyopo anakutana naye mara kwa mara. Mfano kazini, na kila anapokutana naye humpa sifa anayostahili kwa vitu vidogo ambavyo wewe umekuwa ukivipuuzia, hiyo inaweza kuwa kengele ya kwanza ya hatari dhidi ya uhusiano wenu.
Makala Dar24
2. Mawasiliano 
Mawasiliano ni msingi mkuu wa uhusiano wowote ule. Lakini kwa uhusiano wa mapenzi, mawasiliano ni ‘moyo’. Mawasiliano ndiyo yanayokuweka karibu sana na mpenzi wako. Kwa lugha ya kiingereza, mawasiliano huongeza ‘intimacy’.
Unapopunguza mawasiliano ya karibu na mpenzi wako, ni hatari hasa kama kuna mtu ambaye amekuwa akimfuatilia kwa karibu huku akiwasiliana naye hata kama ni kwa mambo ya kawaida lakini mara kwa mara. Hata kama mtu huyo atakuwa akizungumza naye kuhusu vitu vya kawaida kabisa ambavyo wewe unaona uko bize sana huwezi kuongea naye kwa wakati huo kwa kuwa tayari ameshakuwa wako. Jamaa anaweza kuwa anaongea naye kuhusu ‘filamu’ aliyoiona siku hiyo, jinsi alivyochukizwa na foleni ya barabarani, chakula alichokula siku hiyo, ugumu wa kazi aliokutana nao, vituko vya kwenye mitandao ya kijamii n.k.
Mwanamke akiendelea kuendekeza mawasiliano ya karibu sana na mtu huyo ambaye ameshaonesha nia ya kutaka kuwa naye mwanzoni ila wewe ukaonekana kuwa kikwazo, anaweza kujikuta anampa nafasi taratibu bila hata yeye mwenyewe kufahamu. Ataanza kuona anammiss wakati mwingine asipowasiliana naye. Nafasi unayoicha, inaweza kumfanya mrembo wako mwenye msimamo kutetereka kwa kuwa sikio lake linaisikia sauti fulani zaidi ya sauti yako.
3. Kauli zako
Unapokuwa unaongea na mrembo wako unapaswa kuyahesabu vizuri maneno yako. Hasa pale mnapokuwa na mgogoro, chagua kwa umakini maneno ya kumwambia wakati mnamgombana. Unaweza kuwa unaongea kwa hasira, lakini unapaswa kufahamu kuwa maneno yale yanamuingia na yatajirudia kichwani baadae akiwa ametulia hata kama mmeshasuluhisha. Epuka kumuita ‘malaya’, ‘mjinga’, ‘mpuuzi’, ‘unajidai..’ na mengine kama hayo. Haya yanaweza kuchangia sana kumfanya ahisi ndivyo unavyomchukulia.
Endapo utaendelea kuyatumia maneno yanayouchoma moyo wake mara kwa mara mnapopishana kauli, kuna uwezekano mkubwa sana akawa anapata faraja kwa kuongea mambo ya kawaida tu na mwanaume mwingine ambaye siku zote amekuwa akimfuatilia na kumsifia. Hiyo ni kengele ya hatari kwenye uhusiano wenu, muda wowote unaweza kutokea usaliti kama hautajirudi mapema.
fight
Mwanamke hupenda kuambiwa kile anachotaka kusikia. Kumbuka maneno matamu ndio kitu ambacho kila mwanamke anapenda kusikia kikitoka kinywani kwa mpenzi wake. asipoyapata hapo kwa muda, masikio yake hufunguka upande wa pili na kuwa hatari kwa uhusiano wake.
Kumbuka kila mwanamke anapenda kusifiwa, kuambiwa amependeza pale anapohisi amependeza. Anapenda kusifiwa kwa mawazo mazuri anayotoa, jinsi anavyofanya kazi zake na mengine. Hayo asipoyapata kwako na bahati mbaya akawa anapata kauli mbaya, huku kuna anayempa sifa hizo, lazima kengele ya hatari ilie sikioni kwake.
 4. Mabadiliko hasi
Mapenzi yana hatua kadhaa, huanza kwa kasi ya ajabu na kupanda hadi kwenye kilele cha mafanikio ya uhusiano (climax). Lakini hatua hiyo huwa mtihani mkubwa sana kwa kuwa kinachofuata baada ya hapo ni kuendelea kuimarika au kuporomoka taratibu.
Endapo utauruhusu uhusiano wenu kuanza kuporomoka, mshindani wako anayechipukia anaweza kuwa anabidii kali na ushawishi wa kasi ya mapenzi yanayochipukia.
Hivyo, msimamo wa mpenzi wako unategemea pia jinsi wewe utakavyokuwa unajitahidi kuimarisha mapenzi yenu. Fikiria, je, wewe ndiye mtu wake wa kukimbilia kila anapohitaji kushauriwa kitu kama zamani, kuzungumza, kumpeleka sehemu anazopenda na mengine kama ilivyokuwa zamani? Kama sio, fikiria atadumu vipi na msimamo wake endapo atapata mbadala wa kirafiki?
Mwanzo wa uhusiano unaweza kuwa ulikuwa mtu wa kumpa zawadi mara kwa mara, hata kama ni zawadi za kawaida na zisizo na gharama kubwa. Lakini muda unavyozidi kwenda unapunguza au unaacha kabisa. Jukumu hilo linaweza kuhamia kwa mpinzani wako anayeanza na uhusiano wa kirafiki. Hivyo, anaweza kuuteka usikivu wa mrembo wako taratibu na kupelekea kengele ya hatari kulia kichwani kwake. Anaweza kumuonea huruma kwa kumuona mtu mwema sana na anaemjali.
5. Uaminifu 
Unataka mpenzi wako awe mwaminifu sana kwako? Anza wewe kuwa mwaminifu. Na sio tu kuwa mwaminifu, lakini uoneshe kuwa wewe ni mwaminifu.
Uzoefu unaonesha kuwa moja kati ya sababu za wanawake kuwasaliti wenzi wao ni kulipa kisasi kutokana na kuhisi wameonewa. Mrembo anapoamua kuwa na msimamo kwa ajili yako, anategemea wewe uwe na msimamo pia kwa ajili yake pia. Anapoona wewe unatoka nje ya msitari, ndipo huanza kufikiria kuwa huenda msimamo wake ni ‘ushamba’ tu.
6. Kuishi kwa Mazoea
Penzi ni kitu nyeti sana kinachotakiwa kuchukuliwa kwa umakini mkubwa sana. Ni zaidi ya ua linalochipua, unapaswa kulimwagilia kwa mbwembwe za ubunifu kila dakika ili listawi vizuri. Ubunifu unapopungua, taratibu penzi nalo linaporomoka.
Kibaya zaidi, kuishi kwa kuzoea kuwa huyu ameshakuwa wangu hakuishii kwenye maisha ya kawaida tu, mara nyingi kunahamia hata kitandani ambapo unaweza kujikuta unapunguza zile mbwembwe za mwanzo ulizokuwa nazo.
Girls
Hii ni zaidi ya hatari kwenye uhusiano wako. Endapo mrembo wako ataanza kukutilia shaka na kuhisi kuna vitu umevipotezea, anaweza kukwambia au kukaa kimya na kubaki na kiu yake. Mazoea hayo yakikutana na ushindani wowote wa mbwembwe za msaka tonge kutoka upande wa pili, hugeuka kuwa kengele ya hatari pia kwenye uhusiano wenu inayoweza kusababisha usaliti.