NAKUKARIBISHA kwa moyo mkunjufu kwenye safu yetu maalum kwa ajili ya kupeana ujuzi katika anga ya sanaa ya mapenzi. Ni imani yangu, umekuwa ukipata maarifa mapya kila siku kupitia hapa. Kaa tayari uvune kitu kipya leo.
Kwanza kabisa, napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wote ambao mmekuwa mkiwasiliana nami kwa njia ya simu na kunipongeza, kunikosoa na kuuliza maswali kuhusu mambo mbalimbali yanayowakabili katika uhusiano. Kufanya kwenu hivyo kunanipa moyo kwamba, ujumbe unawafikia vilivyo.
Sasa twende moja kwa moja kwenye mada yenyewe. Nazungumzia juu ya mambo ya kuzingatia kama unahitaji kudumu katika uhusiano ulionao. Hapa naomba nizungumze na wanawake zaidi. Nasema hivyo kwa sababu wao ndiyo wanaokumbana zaidi na matatizo ya kuachwa na wapenzi wao kuliko wanaume.
Ni sahihi kusema, wanawake ndiyo huumizwa zaidi katika mapenzi kuliko wanaume. Hii ni kutokana na sababu kubwa mbili; kwa kawaida wao ndiyo hufuatwa na kutongozwa na wanaume, lakini lingine ni kwamba, mara nyingi wanaume ndiyo hutoa uamuzi wa kuacha au kuachana.
Kwa sababu hizo, hakuna ubishi kuwa wanawake ndiyo welengwa wakubwa wa mada hii. Rafiki zangu, kuna mambo kadha wa kadha ambayo yanaweza kusababisha uhusiano kuwa butu na baadaye kuishia njiani.
TAMBUA THAMANI YAKO
Ili uweze kuwa bora ni lazima uanzie kwako, ujitambue kama mwanamke na thamani yako kwa mwanaume wako. Ukiijua thamani yako, lazima utakuwa makini na kila kitu. Rafiki yangu, ninaposema thamani ninamaanisha kwanza kujiamini na kujipa nafasi ya kwanza.
Uamini kwamba wewe ni mwanamke mrembo na unayevutia. Imani hiyo ikishaingia, tayari utakuwa unajali mambo mengi ya msingi, ikiwemo usafi wako binafsi. Waswahili wanasema, mwanamke ni pambo la nyumba. Pambo haina maana ya ua, inamaanisha ule usafi wa kila kitu.
Kwamba nyumba bila mwanamke haiwezi kukamilika, wewe kama mwanamke unatakiwa kufahamu wewe ni kila kitu ndani ya nyumba. Umakini wako na kujitambua ndiyo vitu vitakavyokuweka katika nafasi nzuri ya kudumu katika uhusiano wako na baadaye kuingia kwenye ndoa.
TAMBUA THAMANI YAKE
Ukiijua thamani ya mwanaume kutoka ndani ya moyo wako ni wazi kwamba hata vipengele vifuatavyo hapa chini havitakuwa vigumu kwako kutekelezeka. Inakupasa ujue thamani ya mwanaume wako ipasavyo.
Hilo si tu kwa maneno, bali ni jambo ambalo linatakiwa kufanyika kwa ridhaa ya moyo wako. Ni rahisi zaidi jambo hili kufanyika ikiwa utakuwa na mapenzi ya dhati. Mpende kwa moyo wako wote na ujue kuwa maisha yako yanakamilishwa na uwepo wake.
Ndiyo! Yanakamilishwa na uwepo wake, maana una mategemeo ya kuingia katika ndoa naye. Hapo mtakuwa mwili mmoja na maisha ya kila mmoja yatamtegemea mwenzake.
MHESHIMU
Mwanaume anapenda sana kuheshimiwa na mpenzi wake. Mwanaume akigundua haheshimiwi au unafanya hivyo kwa kumridhisha tu na si kutoka moyoni, ni rahisi kukuacha.
Kama kichwa cha familia, lazima apewe nafasi ya kutoa uamuzi tangu mapema. Ikiwa utakuwa na majibu mabaya kwake, humheshimu ni wazi kwamba atakuacha mapema, maana utakuwa umepoteza sifa za kuwa mama wa familia.