Thursday, November 9, 2017

JINSI YA KUEPUKA INGIA KATIKA NDOA AU MAHUSIANO MACHUNGU

Imewahi kusemwa kuwa ‘You are what you think’ , yaani unavyofikiri ndivyo utakavyokua. Hii ni kweli hata katika mahusiano. Namna tunavyofikiri kuhusu sisi wenyewe na aina ya wapenzi tunaowataka ndivyo inatupelekea kuwa katika mahusiano machungu au ya furaha.
Katika makala hii nazungumzia baadhi ya sababu au malengo ya kuingia katika uhusiano ambayo huchangia watu kujikuta kuwa katika mahusiano machungu.

Mwanamme anataka mwanamke wa aina gani ?

Kwa baadhi ya wanaume mwanamke ni kama mfanyakazi wa ndani –ila zaidi ya mfanyakazi ni wa kuwazalia watoto na kulea. Kwa wengine ni chombo cha starehe,wakitilia maanani uzuri wa sura na umbo.

Mwanamke anataka mwanaume wa aina gani ?

Kwa baadhi ya wanawake , mwanaume ni tiketi ya 'kutoka ' kimaisha. Ni mlezi baada ya baba na mama yao. Mwanaume ni wa kumrahisishia maisha na kumfanya apumzike kuwaza na kuhangaika katika mihangaiko ya kila siku.
Na bahati mbaya wapo wanawake wengi huingia katika mahusiano ambayo wanajua wazi wao hawawezi kuwa washirika wa kweli wa waume zao. Ila wanaona ni poa kuwa hawataki shida, kwani anaonekana mwanaume anao uwezo wa kumtunza  na kumrahisishia maisha.
Wanawake wa aina hii wanaangalia upande mmoja tuu  wa mahusiano, yaani namna gani wao watanufaika kwa ‘kulelewa’  vizuri na mume, na sio kwa namna gani wao pia watakua wa msaada kwa mwanaume husika –msaada kimawazo, kimazungumzo, na haswa haswa kwa ndoto ambazo mwanaume ameweza kushea nae.
Matokeo ya malengo mabaya ya aina ya mwenza unayehitaji

Kwa watu wa mtazamo wa hivi, wanajikuta wakiingia katika mahusiano bila  muunganiko haswa wa ushirika unaowafanya kuwa mwili mmoja kwa mpangilio wa maisha ya mapenzi yenye furaha na hatimaye  ndoa yenye furaha.
Hivyo watu wanaanza mahusiano na kuingia katika ndoa , lakini kiukweli hakuna ushirikiano na umoja unaotakiwa wa maisha ya furaha. 
Mwanaume akijua wazi kuwa hana mshirika anakubali kuingia katika ndoa pengine kwa misukumo ya kifamilia, au kwa sababu anazoona za ‘kiusalama’ kuwa kwa kuwa na mke wa hivyo , yeye atakuwa na nguvu sana juu yake, hivyo hakutakuwa na sababu ya mwanamke kutoka nje ya ndoa, na yeye mwanaume atakua na uhuru wa ‘kucheza’.  
Pengine mwanaume aliumizwa katika mahusiano yake yaliyopita wakati hana uwezo wa kifedha au hakuwa na sauti katika mahusiano hivyo anajiona njia ya kuwa salama ni ya kuwa na mwanamke ambaye wana ‘gepu’ kuwa na yeye ndo atasikilizwa.
Kutokuwepo kwa usawa au ushirikiano wa karibu kama washirika katika mahusiano au ndoa, kunafanya wawili hao ingawa wapo pamoja muda mrefu , pengine wanaishi nyumba moja , wakawa wako mbali kimauhisano kwakua ‘hawazungumzi lugha moja’. 
Wapenzi wanakuwa na mahitaji mengi ambayo hayakamilishwi na uhusiano walio nao, na uvumilivu wa kukubali kutokukamilika huko ni mgumu hivyo anayeumia zaidi kwa kutokukamilika mahitaji yake, anatoka nje ya uhusiano ili kuziba pengo.
Hata hivyo kutoka huko hakuleti furaha ya kweli kwa muhusika kwani tayari amekwishajikomit kwa mwenza fulani, kinachoendelea ni kua wakati akitafuta furaha ya muda mfupi, anasababisha maumivu makubwa kwa mwenza wake na kwake mwenyewe, na pengine kwa watoto kama wana watoto.
Hitimisho

Una muda mrefu wa kuchagua na kumchunguza mwenza unayemtaka. Usikubali kuingia kwa mahusiano ya kudumu na mtu ambaye baada ya kujichunguza wewe mwenyewe unaona kabisa si mshirika unayehitaji. Usilazimishe mahusiano kwa kuangalia ‘faida’ na nafasi ya mtu fulani.

Kuvutiwa kihisia za kimapenzi na kufanya mapenzi hakutoshi kukujulisha kuwa unampenda mtu. 
Na hata kama unampenda , kumbuka muda mwingi wa uhusiano wenu mtautumia bila kufanya mapenzi au kuwa karibu kihisia. 
Unahitaji kumkubali mwenza wako zaidi ya unavyomkubali kimapenzi.