Tuesday, October 31, 2017

Usimng’ang’anie asiyekupenda, Angalia thamani yako



Ili mapenzi yaweze kuwa bora kwa kila aliye katika mahusiano, huwa ni vyema kila mmoja kuiona thamani ya mwenzake. Ukipenda kujiangalia mwenyewe  si ajabu mwenzako kupata hisia za kuwa humthamini wala humjali.
Muunganiko wenu katika mapenzi maana yake tayari mmekuwa kitu kimoja. Katika mimi unaweka sisi.
Ila pia ni vyema ikakumbukwa ladha na maana halisi ya mapenzi ipo kwa anayekupenda na kukuthamini. Unapokuwa na uhakika kama anakupenda na kukuthamini hapo ndipo nafsi yako itatulia na kuwa na amani. Ndani ya mapenzi na mtu wa aina hii ni amani na utulivu kwa kwenda mbele. Hakuna majuto wala majonzi ya kila siku.
Unapoamua kuwa katika mahusiano na mtu ambaye hakupendi, bali unakuwa naye kwa kuwa tu unampenda jua umejiingiza katika utumwa. Mapenzi ni suala la kihisia zaidi. Mwenzako anapokosa hisia na wewe maana yake hata uwepo wako hauthamini inavyopaswa. Na hapo ndiyo tunaona yale mahusiano ya kingono yanapozaliwa na si ya kimapenzi kwa maana halisi.
Yaani mwenzako anapokuwa na mihemko ya kingono ndipo anapokutafuta na si vinginevyo. Niliwahi kuongea na msichana mmoja aliyewahi kuniambia anampenda kijana mmoja ambaye anauhakika kabisa yeye hampendi. Alinambia uhakika huo kaupata kutokana na kijana huyo kumtakia  kuna msichana yupo anampenda na kumjali ila si yeye.
Kuonesha zaidi kumpenda msichana yule mwingine, jamaa aliwahi kumwambia kama ikitokea hata huyu msichana akagombana na yule mpenzi mwingine wa yule jamaa, kijana yule alikuwa radhi kumdhuru huyu msichana.
Hata kwa matazamo wa haraka hapo unaweza kugundua ni kwa namna gani huyu msichana alikuwa haitajiki. Ila cha kushangaza msichana huyu(aliyeongea na mimi) alimwambia mvulana husika yuko radhi kuwa naye hivyo hivyo.
Aliamua kuwa hivyo akiamini ipo siku jamaa atamuelewa. Kweli walikuwa pamoja. Ila  unajua kinachomkuta sasa?
Kila jamaa anapogombana na yule msichana mwingine anamtumia huyu kingono na mambo mengine yasiyo ya kimapenzi, na bila kutafakari mara mbili huyu msichana anafanya kwa kile anachoamini hali hiyo itamfanya huyu jamaa amfikirie zaidi. Kuna kitu cha kuangalia hapa.
Suala la mapenzi si suala la kuoneana huruma wala aibu. Mapenzi ni hisia. Unapojitoa kwa mwenzako kwa kila jambo na unamuona haelekei ujue hana hisia na wewe. Kwanini unakubali kuteseka na kuumia kila siku kwa kumuangalia yeye tu?
Ndiyo, unampenda sana, unamjali sana na unamuhitaji sana, ila kama yeye hakutaki wa kazi gani? Ni muda wa kujiangalia na wewe sasa.
Ona thamani yako kama binaadamu, jionee huruma jinsi unavyoteseka kila siku kwa mtu asiyeona thamani yako.
Wewe ni binaadamu mwenye hadhi na thamani, bila kujali muonekano wala rangi yako. Unahitaji mwenye kukuthamini na kukujali na si anayekufanya kama mdoli wake ngono au kadi yake ya pesa. Kataa utumwa wa mapenzi kwa kuiona thamani yako.
Ni vyema ukalia kwa kumkosa kuliko kuonekana unaye wakati moyoni siyo wako. Hakuna sifa ya kuwa na mtu mwenye fedha au muonekano mzuri ikiwa hakujali wala haupo moyoni mwake. Mapenzi ni amani na raha.
Mapenzi hufanya watu wafurahi na kusahau shida zao. Ila jiulize kwanini kwako hayako hivi? Unaenda kwa mwenzako badala afurahie uwepo wako, yeye anaona unajipendekeza. Unampigia simu na kumpa maneno mazuri ya faraja, yeye anaona unamsumbua. Sasa wa kazi gani? Siku njema wapendwa.