Baada ya kuidadavua mada ya ‘ Hisia zinaweza kukugeuza katuni mapenzini’, leo tunapiga bao kwingine na kuibuka na somo safi kabisa ambalo linatanguliwa na kichwa kinachosema “Uchawi mdogo, unaoweza kudumisha penzi lako.”
Ni mada yenye maana kubwa na nina uhakika kuwa baada ya kuimaliza, utakuwa umeshapata mwanga wa kutosha wa kujua jinsi ya kulinda uhusiano wako usiende na maji. Uchawi wenyewe ni kitu kidogo ambacho wengi wanakidharau, ingawa kina maana kubwa.
Uchawi wenyewe ni uoga. Tafsiri ya uoga ni hali ya kutokuwa na ushujaa wa kufanya jambo fulani. Tafsiri hii, ndiyo inayowafanya watu waikatae sifa hii. Wengi wanapenda waonekane ‘ngangari’, wenye msimamo usiyoyumba katika suala zima la uhusiano wa kimapenzi.
Si kauli ngeni kwa baadhi yetu kujisifu kwamba hatuwaogopi wapenzi wetu na kwamba sisi ndiyo vichwa. Tambo za aina hii, anaweza kusema mwanaume ama mwanamke, lakini je, anayetoa matamshi ya aina hii anakuwa amepata wasaa wa kutafakari athari iliyo nyuma ya sentensi yake?
Kwa kusema ule kweli, mtu anayesema hamuogopi mpenzi wake ni sawasawa na anayejikaanga kwa mafuta yake mwenyewe. Mwenzi wa mtu, anayetoa kauli ya aina hii, mara anapopata bahati ya kusikia kinachozungumzwa na mwenzake, anaweza kuchukua uamuzi ambao awali hakuufikiria.
Kama si kuamua kutengana, basi anaweza kujivalisha ‘undava’. Akishakuwa katika hali ya aina hiyo, maana yake hakutakuwa na mdogo, wala anayekubali kujishusha kwakuwa kila mtu atasema ‘kama noma na iwe noma’. Picha ikishasomeka hivyo, basi hapo hakuna penzi tena.
Kwanini nasema uoga ni uchawi mdogo, unaoweza kudumisha penzi lako? Jibu lake ni kwamba mtu muoga maana yake ataishi kwa mipaka, huku akiwa na tahadhari ya hali ya juu kwa kuhakikisha kwamba anakuwa na maelewano mazuri na mpenzi wake.
Atakuwa akiishi, huku anapingana na nafsi yake kufanya yale ambayo yatamkwaza mwandani wake, hiyo husaidia kuondoa migogoro kati ya wawili wapendanao, hivyo kuchagiza amani na upendo.
Anayefanya jitihada za kudumisha maelewano na mpenzi wake ni sawa na anayepalilia shamba lake, kuliwekea mbolea pamoja na dawa za kuulia wadudu kwasababu mafanikio yao ni kuvuna mavuno bora.
Ukiwa muoga, hautothubutu kumdharau mpenzi wako, hautojitapa mbele ya marafiki zako kwamba hawezi kukufanya jambo lolote. Badala yake, utanyenyekea pale panapostahili, hivyo kuzidi kustawisha penzi.
Pia, ni vizuri kukumbuka kuwa utiifu ni chachandu ya uhusiano wako.
Uoga ndiyo unaoleta utiifu, na wapenzi wanaoheshimiana huishi kwa kujali hisia za wenzi wao. Mtu anayejiheshimu, siku zote atakuwa anapigania uhusiano wake uwe wa kudumu, hivyo ataishi tahadhari ya kutomuudhi mwenzake.
Ninaposhauri uoga, haina maana ndiyo ukose uhuru ama ushindwe kujiamini. Mtu sahihi katika uhusiano wake ni lazima ajiamini, pia awe na uhuru wa ‘kuinjoi’ katika penzi lake. Kwa mantiki hiyo basi, jambo ambalo ninalolishauri hapa ni kuwa lazima kuwepo mipaka ya kihisia kati ya mtu na mpenzi wake.
Uhuru wenye mipaka ni pointi nyingine ya kuelekea kwenye uoga. Maana ya kusema hivyo ni kuwa unapojiamini kasha ukawa huru, lakini ukajenga misingi ya heshima kwa yule umpendaye, itakusaidia kuupa afya uhusiano wako.
Ukimuogoa mpenzi wako, maaana yake utakuwa tayari kumsikiliza wakati wowote. Atakapokushauri, utamjali na kuzingatia ushauri wake kabla ya kuufanyia kazi. Kinyume chake, utamdharau na kumuona wa kazi gani, kwahiyo chiochote atakachokuambia utakiona ni pumba tupu.
Lazima ujiamini katika mambo chanya. Mfano umegundua mpenzi wako ana tabia zisizofaa, hivyo unaamua kusimama imara ili dharau isivuke mpaka. Jiamini na usimame imara katika kuzuia matumizi mabaya ya pesa aliyonayo mpenzi wako na vitendo vingine ambavyo havikupendezi.
Hata hivyo, ni vizuri pia ukikumbuka, kikomo cha uhuru wako ndipo uhuru wa mwenzako unapoanzia.
Maandiko matakatifu yanasema: “Mwadamu aliye na hofu ndiye anayempendeza Mungu.” Pia na mimi nakandamiza kwamba ukiwa na uoga kwa mpenzi wako, ndivyo utakavyomfurahisha na kumfanya aendelee kukuona bora zaidi.
Akikuona bora, siyo ndiyo utakuwa umroga mpaka asifikirie kuachana na wewe? Na huo si ndiyo uchawi wenyewe? Kwa leo inatosha. Tukutane Jumatatu ili tuendelee kufanya maajabu ya Love and Marriage.