Monday, October 30, 2017

Tambua Jinsi Ya Kuongeza Mvuto Kwa Mpenzi Wako



Kama umeshushwa thamani unakuwa kwenye hatari ya kuachwa. Hata kama mwenzako alikuwa ameshafikiria suala la kuingia kwenye ndoa na wewe lakini kwa sababu ameshakushusha thamani ndoa inaweza kuyeyuka.
Ukiwa kwenye ndoa ni hatari zaidi maana mwenzako hukuchukulia wa kawaida – mazoea huzidi na hapo ndipo uhitaji wa kuwa na mwingine wa pembeni unapoanzia. Haoni cha muhimu tena kwako, ndiyo maana wazo hilo huvamia ubongo wake kwa kasi sana.
Itafikia hatua, kama upo ndani ya ndoa, mwenzako atagoma kuongozana na wewe na kama ikitokea hivyo mkikutana na rafiki zake njiani hatakutambulisha. Hisia kwamba hamuendani humwingia.
UNAFANYAJE SASA?
Kubwa unalotakiwa kufahamu rafiki yangu mpendwa, suala la kupanda au kushuka thamani lipo mikononi mwako. Yapo mambo ambayo ukiyazingatia, mwenzako hawezi kukuchoka na kufikia hatua ya kukushusha thamani.
Tayari tumeshaona athari zake lakini hapa sasa nataka kukupa mbinu ambazo ukiwa nazo makini basi itakuwa rahisi kwako kubaki namba moja na mtu muhimu zaidi (ndiyo inavyotakiwa kuwa) kwa mpenzi wako maana ni haki yako.
ANZIA MWANZO
Ni rahisi zaidi kulinda thamani yako kuanzia mwanzo wa uhusiano wenu. Ikiwa tayari mmeshakomaa halafu tatizo hilo likajitokeza, hutumika nguvu nyingi zaidi kulirekebisha kuliko kujizatiti kuanzia mwanzo wa uhusiano. Ni mambo gani hayo? Twende hapo chini.
CHUNGA KAULI ZAKO
Naomba ieleweke wazi kuwa mada hii ni maalum zaidi kwa wanawake. Kitu muhimu cha kwanza kabisa kwa mwanamke ambaye anataka kuilinda thamani yake kwa mpenziwe ni kupima sana kauli zake.
Acha kuropoka hovyo, pima maneno yako na ikiwezekana kama unadhani kuna jambo huna uhakika nalo usizungumze kabisa. Katika eneo hili, uwe makini zaidi mnapokuwa na watu wengine. Kama mwanamke usiwe mchangiaji hoja sana.
Utulivu wako unaweza kuwa silaha kubwa ya kukufanya ubaki na thamani yako kama mwanamke anayejitambua.
USIRUHUSU MAPENZI
Msichana mwenye kujitambua na kufahamu thamani yake sawasawa hawezi kuruhusu mwili wake ujulikane na mwanaume harakaharaka. Onesha unajitambua na usikubali kirahisi kuuacha mwili wako uchezewe.
Mpe hoja; kwanza mapema, hajakuoa wala kukuchumbia, haraka ya nini? Wakati unawaza kuhusu kutoa penzi lako, lazima ufikirie kuhusu athari zinazoweza kukupata kwa kukurupukia mapenzi. Mwanaume ambaye bado hamjachunguzana na huna uhakika naye wa kutengeneza maisha, kichwani mwake hakuweki kwa asilimia kubwa.
Ukumbuke kwamba, ukipata matatizo yoyote – binafsi au yanayosababishwa na uhusiano wenu, anakuwa hana uwajibikaji wa asilimia kubwa kwa tatizo hilo. Utabaki wewe na matatizo yako!