Friday, October 13, 2017

Kama Una Tabia ya Kuchepuka Soma hapa

Kuna hiki kidude ambacho siku hizi karibu kila mtu anacho. Wakubwa wadogo, wazee na vijana, wake kwa waume, lakini kimekuwa ni shiiida. Kinasumbua sana watu wengi.  Mtu unakuwa huna raha kabisa shauri ya kidude hiki? Jamani Why?
Kidude hiki kimekuwa kikirahisisha hata waliokuwa hawajui kuongea, sasa wanaweza kujieleza kwa ufasaha. Kidude hiki kinaitwa simu ya mkononi. Pamoja na kuwa simu inawezesha mambo mengi lakini pia imewezesha kukua kwa umiliki na uendeshaji wa taasisi ya michepuko.
Lakini pia kumeongezeka na matatizo mengi ya uendeshaji wa taasisi hii mpya. Hapa naona ni vizuri kutoa mwongozo wa matumizi ya simu kwa wale waliomo kwenye taasisi ya michepuko.
Mtu anakuwa na mchepuko wake na sijui kwa nini, lakini michepuko ina tabia ya kuwa haina taimingi, pale mwenza ndo uko naye, mchepuko ndo unapiga simu. Kumekuwa na njia mbalimbali za kuepukana na adha hii, wadau wengine huweka simu silent, wengine vibreshen, ushauri wa kitaalamu unasema chondechonde usiweke kwenye vibreshen, wenza wote wana machale kishenzi, lazima utasikia ‘nani huyo? mbona hupokei?’
Maswali haya ni hatari sana usikubali yakutokee, hivyo daima weka simu  kwenye silent. Japo tatizo la michepuko mingine usipopokea ndiyo haachi kupiga, unakuta missed call 20 saa saba ya usiku.
Ukiwa na mchepuko we sevu jina lake mjomba, au shangazi au ba mdogo, usiandike fundi majeneza au fundi pikipiki, imeshapitwa na wakati hiyo, utashtukiwa. Ni vizuri ukiwa peke yako kufanya mazoezi ya kuekti kwenye kioo unapokea simu, ili wakati unasema uongo uso uwe umetulia kabisa wakati unajibu uongo, maana unaweza kulazimika kupokea simu ya mchepuko, mwenza yuko mbele yako, ikalazimika uanzishe kujibu simu za kujidai unaongea biashara ya kulipia kontena uliyotoa bandarini kimagumashi, au pengine kujidai unaongea na muuza mawigi ya Brazili, hapo lazima uekti vizuri kuliko msanii wa Bongo Muvi.
Ili kupunguza mitihani hii, jamaa yangu mmoja wa Kiluvya amempangia mchepuko muda wa kupiga simu hii imemuondolea adha ya kulazimika kupokelea simu chooni na bafuni.  Kwa hiyo tafadhali wandugu, tena chonde sana yale mnayochati futeni, hata kama lilikuwa neno tamu kama I love you my Chokoleti futa usitake sifa ya kuliacha kwenda kuonesha wenzio, litakukosti ohoo.
Amri kuu ya simu ukiwa na mchepuko ni kuwa unatakiwa kuibeba popote utakapokuwa, bafuni chooni, msibani harusini usingizini, ukimuachia nafasi mwenza aibebe umekwisha. Pia kama una mchepuko ni muhimu sana umpe semina elekezi, warsha na kongamano  kuhusu nini cha kusema ikiwa kwa  bahati mbaya simu ikiangukia mikononi mwa mwenza wako.
Asianze samahani nimekosea namba, hiyo imepitwa na wakati.