Monday, October 9, 2017

JE, UNATAKA KUMUACHA MPENZI ASIYE CHAGUO LAKO? FUATA HATUA HIZI.

KUNA wakati kwenye mapenzi, inafikia hatua mtu akahisi amemchoka mpenzi wake. Kuna mambo mengi, lakini kubwa ni kwamba, anajikuta ameanza kufikiria kwamba, kumbe mwenzi aliye naye si sahihi kwake na hataki tena kuendelea naye. 
Hili ni jambo la kawaida kwenye uhusiano. Rafiki zangu, angalizo moja muhimu katika mada hii ni kwamba, wale ambao tayari wapo kwenye ndoa, mada hii haiwahusu kabisa. Hapa nazungumza na walio kwenye uhusiano wa kimapenzi (pengine hata kwenye uchumba hawajafika).
Mapenzi ni hisia za ndani, uamuzi wa kuendelea na mtu katika hatua ya uchumba ambayo huambatana na ndoa ni uamuzi wa ndani wa mhusika mwenyewe. Hakuna wa kumshikia fimbo kumlazimisha.
Mnapokuwa kwenye uhusiano ni kipindi chenu cha kuchunguzana sana. Kila mmoja lazima amjue mwenzake sawasawa, hii itamsaidia kila mmoja kufahamu anakwenda kuingia kwenye ndoa na mtu wa aina gani.
Hapa nazungumzia eneo la KUACHANA. Ni kweli, umegundua kwamba hakufai (kwa sababu zako binafsi) ambazo kwa hakika huwezi kumweleza, lakini mwenzako ndiyo kwanza anaonekana amefika – hafikirii kuachana na wewe.
Inawezekana umejaribu kupima sababu zako na ukagundua ni za ‘kijinga’ ambazo huwezi kumwambia mpenzi wako, lakini MOYO wako umekuthibitishia kwamba huyo si CHAGUA lako na uking’ang’ania kuendelea naye basi FURAHA katika maisha yako itakuwa ni sawa na kitendawili kigumu mno.
KWANINI UNATAKA KUMWACHA?
Hii ni hatua ya kwanza rafiki yangu. Lazima ujiulize, ni kwa nini unataka kumwacha? Kama nilivyosema awali, ni vyema kuuchunguza moyo wako, maana isije ukamwacha kwa sababu ya tamaa zako au umeleweshwa kimapenzi na mwingine, ukashawishika kwa nje – baadaye utajuta.
Sababu kubwa ya kuachana kwenu inatakiwa iwe ile ya kutafuta amani ya moyo wako, maana umeshajichunguza na umegundua kwamba, kulazimisha kuendelea naye, maana yake utaishi maisha yasiyo na amani.
Kama ndivyo, wazo hili ni sahihi, lakini kumbuka hutakiwi kumwumiza mwenzako wakati ukitekeleza jambo hili ambalo ni matakwa yako binafsi.
SABABU ZINAZUNGUMZIKA?
Zipo sababu kuu mbili za kutaka kusitiza uhusiano. Ya kwanza nilishaifafanua kwenye kipengele kilichotangulia, lakini ya pili sasa ni kama kweli ana kasoro ambazo unaweza kumweleza moja kwa moja.
Kumbuka njia nitakazokufundisha hapa ni za muda mrefu, zinahitaji ufundi na inategemea na namna mwenzako atakavyopokea, hivyo kama unajua mwenzako hajatulia na ushahidi unao, mwekee mezani kuliko kumzungusha.
Ikiwa kipengele hiki hakikuhusu, basi twende wote hatua kwa hatua katika vipengele vifuatavyo;
PUNGUZA MAWASILIANO
Silaha ya kwanza ya mapenzi ni mawasiliano. Kuwasiliana ndipo kunapodumisha penzi. Hili lilikuwepo toka enzi na enzi, ingawa kwa sasa kuna maendeleo ya utandawazi, mawasiliano yamekuwa rahisi zaidi.
Punguza kumpigia simu, kumwandikia meseji au waraka pepe. Akikupigia yeye pokea, akituma meseji unaweza kujibu na wakati mwingine kuacha. Akikuuliza, mwambie una mambo mengi. Hii ni alama ya kwanza itakayomfanya ahisi uhusiano wenu umeanza kuyumba.
PUNGUZA MAHABA
Mahaba ni kati ya nakshi za uhusiano, kupoteza au kupunguza mahaba humaanisha kwamba kuna jambo jipya limetokea. Sasa punguza mahaba. Kwa mfano, akikutumia meseji na kukuita kimapenzi dear, sweetie nk, wewe mjibu kwa kumwita jina lake.
Ikiwezekana mwite jina lake kamili, mathalani mpenzi wako anaitwa Joseph na umekuwa na kawaida ya kumwita Joe, mwite Josefu – ile ya Kiswahili kabisa, atagundua kuna tofauti. Majina mengine ni kama Margareth – Maggie - Magreti, Erdward – Edo - Edwadi, Abdallah – Dulla – Abdala n.k.
Mwenye macho haambiwi tazama, kwa dalili hizi ambazo utazionyesha hata mnapowasiliana kwa njia ya simu au katika mazungumzo ya mara kwa mara, atagundua kwamba kuna tatizo. Ama amechokwa au anatafutiwa sababu.
Zaidi ya yote atahisi umebadilika na huendani naye kitabia, hivyo atapendekeza muachane, jambo ambalo kwako ni sherehe.
BADILI RATIBA
Ili uweze kufikia lengo lako, ikiwa hatua za awali hazijazaa matunda, sasa badilisha ratiba zako. Kama mlikuwa na kawaida ya kuonana labda kila wikiendi, sasa mwambie una mambo mengi.
Mnaweza kukubaliana kukutana, lakini ghafla unakataa na kusema kuna mambo yameingiliana hivyo hamuwezi kuonana tena. Mabadiliko ya ratiba zako, tena ya ghafla ikiwezekana yawe na maudhi yatamgongea alamu kichwani mwake, kwamba WEWE SIYE TENA!
Cha kufurahisha sasa, yeye ndiye atakayechukua uamuzi wa kuachana na wewe. Hapo utabaki salama, ukisubiri aliye sahihi kwako
Je, ni sahihi ujilazimishe kuwa naye huku moyoni humpendi au uachane naye ili uepukane na matatizo yasiyo ya lazima huko mbele?
Jibu ni rahisi sana; kuachana naye. Yes! Hapo sasa ndipo kwenye mada yenyewe...kama una sababu zinazoeleweka weka mezani, ikiwa huna, vipengele vifuatavyo vinakwenda kukuachanisha naye mara moja na utabaki ukiwa mwenye amani naye akiendelea na maisha yake.
Tuendee sasa...

KATAA MITOKO(OUTING)
Kwa kawaida outing hunogesha penzi. Kama mlikuwa na kawaida ya kutoka pamoja, badilisha ratiba kwa visingizio visivyo na maana. Akitaka mtoke, mtafutie sababu.
Jambo kubwa na muhimu kwako kuzingatia hapa ni kwamba, sababu zenyewe ziwe hazina msingi, kiasi kwamba hata yeye agundue kwamba hutaki tu kutoka naye. Hata kama akiwa na hisia hasi si mbaya sana maana ndiyo lengo lililopo moyoni mwako – akuache!

MSHUSHE THAMANI
Kusifia ni jambo ambalo hustawisha penzi. Bila shaka mara kwa mara umekuwa ukifanya hivyo kwa mpenzi wako. Wakati mwingine, hata kama ni kwa mambo ya uongo, wengi hupenda tu kuwasifia wenzi wao.
Badilisha utaratibu. Sasa mshushe thamani. Unaweza kumwambia: ”Dah! hujapendeza kabisa...siku hizi huwezi kufanya uchaguzi mzuri wa mavazi.”
Kwa kauli hii lazima kuna kitu kitagonga kichwani mwake. Atajua labda una mtu mwingine anakudanganya au umemchoka tu na pengine una dharau. Hayo ni mawazo yake, tena akiwaza hivyo ni vizuri zaidi kwa sababu ni rahisi kutamka: “Kama vipi tuachane bwana..” sasa hapo kuna nini tena zaidi ya kushangilia?

MLAUMU KILA MARA
Chuki na hasira si vitu vinavyokubalika kwa wapenzi. Mara nyingi wenzi huwa na sura zenye bashasha. Wanaoneshana mapenzi na wanajaliana kwa kila hali. Hili ndilo linalotarajiwa na wengi. Sasa wewe ukumbuke kwamba, uko kwenye kipindi cha matarajio ya kuachana naye. Usijali, kwako lawama ndiyo mtaji mzuri. Hata kama akifanya kosa dogo tu, ambalo kwa kawaida mngeweza kulisuluhisha vizuri tu, wewe unamshushia lawama.
Kuna mambo mengine yatakuwa madogo zaidi kiasi cha kumchanganya na kumshangaza, hilo lisikupe hofu, kwa sababu unaijua nia yako.  

SASA ACHANA NAYE!
Kwa vipengele vyote hivyo, lazima atagundua kitu. Jambo la kufurahisha ni kwamba, anaweza kugundua kwamba wewe siye na wala si kwamba unafanya makusudi. Hapo ni rahisi zaidi kwake kujitoa.
Wapo wengine ving’ang’anizi, hawajui kukataliwa. Mkifikia hatua hiyo na bado anaendelea kuonesha uvumilivu, huna haja ya kujitesa zaidi, mwambie ukweli – kwamba ulikosea awali na sasa unahitaji kumwacha huru na maisha yake.
Rafiki zangu ni jambo jema kabisa. Kuna sababu gani ya kuendelea kuwa na mtu ambaye moyoni unajua wazi kuwa huna mapenzi naye? Uamuzi ni wako!