Wednesday, October 18, 2017

Chips Mayai hatari kwa afya yako!?

 

Chips yai...

WATAALAMU wa Kilimo na Afya wamesema kuwa vifo vingi husababishwa na ulaji hafifu wa matunda na mboga za majani huku wakihadharishwa kuwa ulaji wa chipsi mayai unachangia unene unaosababisha vifo vya ghafla.

Katika mkutano wa kwanza wa uhamasishaji matumizi ya bidhaa za matunda na mboga unaofanyika mjini Arusha, wataalamu hao walisema inapotokea vifo vya namna hiyo, baadhi ya watu kusingizia sababu mbalimbali hususani uchawi.

Wamebainisha kwamba watu wengi wanakula matunda na mboga chini ya kiwango cha gramu 400 kilichowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), jambo ambalo ni hatari kwa afya.

Mtaalamu kutoka WHO, Godfrey Xuereb alisema jana kwamba takribani watu milioni mbili hufa kila mwaka kutokana na maradhi yanayosababishwa ukosefu wa lishe za matunda na mboga.

Mwenyekiti wa Baraza la kuendeleza Kilimo cha Matunda na Mboga (Hodect), Felix Mosha alisema viazi vilivyochomwa kwenye mafuta na kuchanganywa na mayai ya kukaanga maarufu kama Chipsi Mayai unaonesha kushika hatamu katika lishe za wakazi wa mijini hasa vijana na wanawake.

Akielezea chakula hicho kama mlo ‘mchafu’, Mosha Alisema: “Matokeo yake taifa sasa limekumbwa na tatizo la unene uliokithiri hasa miongoni mwa watoto na akina mama na kuchangia vifo vingi isivyotarajiwa.” Ofisa kutoka Wizara ya Kilimo na Chakula, Geoffrey Kirenga Alisema:

“Na mara nyingi mtu akionekana mnene huchukuliwa kuwa na afya lakini ukweli wengi huwa na utapiamlo na wanapofariki ghafla wanakuwa chanzo cha uvumi, tetesi na hisia za ajabu wakati chanzo hasa huwa ni ukosefu wa vitamini na madini yatokanayo na matunda na mboga”.

Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe akifungua mkutano huo, alisema wastani wa mtanzania mmoja hula gramu 80 pekee za matunda na mboga kwa siku.

“Hii ni asilimia 20 tu ya kiwango kilichowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) ambacho ni gramu 400 kwa mtu mmoja kwa siku.”

Alisema Maghembe na kuongeza kuwa asilimia kubwa ya Watanzania humaliza hadi miezi miwili bila kugusa hata tunda moja.

“Na hii ni aibu maana hapa nchini kuna matunda ya kila aina ambayo pia hupatikana kwa bei ya chini sana, lakini bado watu hawana mwamko wa kuyatumia kiafya na hata katika mila zingine matunda na mboga huonekana kuwa ni vyakula vya watoto,” alisema Waziri Maghembe.