Monday, June 11, 2018

Yafahamu Makosa Wafanyayo Wapenzi Wawapo Chumbani.

Wapenzi wengi wanaishi kwa mazoea, hawajui nini wafanye na nini wasifanye kwa ajili ya kupalilia mapenzi yao na matokeo yake, inakuwa rahisi mume kumchoka mke au mke kumchoka mume kwa sababu ya vitu ambavyo wahusika wenyewe ndiyo wamevikaribisha.

Yapo makosa ambayo watu wengi wamekuwa wakiyafanya wawapo chumbani na wenzi wao, iwe ni kwa kujua au kwa kutokujua.

Hakuna muda wa muhimu kwa wanandoa au wapenzi wanaoishi pamoja, kama ule muda kabla hamjapitiwa na usingizi. Ukiwa makini, utayafurahia mapenzi lakini ukikosa umakini na kuyafanya makosa yafuatayo, utakuwa unaiua ndoa yako kwa mikono yako mwenyewe.

Yafuatayo ni makosa ambayo wapenzi wengi huyafanya kila siku na kusababisha mapenzi yapungue taratibu:

KWENDA KULALA MUDA TOFAUTI

Yawezekana watu wengi wanalichukulia suala la kila mmoja kwenda kulala kwa wakati wake kama jambo la kawaida. Kwamba wanandoa au wapenzi wanaishi pamoja lakini kila mtu ana ratiba yake ya kwenda kulala, huyu akiwahi leo kupanda kitandani, yule anachelewa, yule akichelewa huyu anawahi, ilimradi tu mnapishana.

Wataalamu wa uhusiano wanaeleza suala hili kuwa sumu kali kwa wapendanao kwa sababu kisaikolojia, unapopanda peke yako kitandani kulala, nafsi inajihisi upweke na taratibu inaanza kujitenga na ya umpendaye.

Mkiendelea hivi kwa muda mrefu, hisia zinapungua na baadaye unaanza kumchukulia mwenzi wako kama mtu wa kawaida tu, ambaye hata asipokuwepo au ukikosa ukaribu wake maisha yako yanaendelea kama kawaida.

Kama na wewe ni miongoni mwa watu wenye tabia hii, badilika mara moja. Hutakiwi kuwa na visingizio katika hili, muda wa kulala ukifika, hakikisha unaambatana na mwenzi wako kupanda kitandani.

Faida nyingine ya kuongozana pamoja kwenda kulala, hata kama kulitokea mikwaruzano ya hapa na pale kutwa nzima, huu ndiyo muda mzuri ambao kila mmoja anaweza kueleza dukuduku lake na kumaliza tofauti kati yenu.


KUWA BIZE NA SIMU AU TV MUDA WA KULALA

Utandawazi umekuja na mambo mengi, simu zenye intaneti (smartphones) zimegeuka na kuwa kero kubwa kwa wanandoa au wapenzi wanaoishi pamoja. Unakuta mume au mke, muda wa kulala ukifika, anapanda kitandani na simu yake.

Badala ya kuwa pamoja na mwenzi wako kwa mazungumzo ya hapa na pale, kubadilishana mawazo na kubembelezana wakati mkitafuta usingizi, unakuta mtu yuko bize na simu, mara aingie kwenye magroup ya WhatsApp, Instagram, Facebook au Twitter. Hakuna tabia inayoweza kukuweka mbali kihisia na mwenzi wako kama hii.

Wengine unakuta anapanda kitandani akiwa na laptop au anawasha TV ya chumbani na kuanza kuangalia movie au tamthiliya. Matokeo yake, unasababisha mwenzi wako akose usingizi mzuri na hata akipata, analala akijisikia vibaya kwa sababu anaona uwepo wake hauna maana yoyote kwa mwenzi wake.

KUWA ‘BUBU’ MKIWA CHUMBANI

Wapo baadhi ya wanandoa au wapenzi ambao wanapoingia chumbani, kila mmoja anajifanya kuchoka sana kiasi kwamba huyu anajitupa kitandani na kugeukia kule, huyu naye anageukia upande mwingine na muda mfupi baadaye, unasikia kila mmoja anakoroma.

Hakuna jambo linalonogesha mapenzi kama mazungumzo ya chumbani wanayoyafanya wanandoa au wapenzi kabla ya kupitiwa na usingizi, Wazungu wanaita ‘Pillow talks’.

Si vibaya kuzungumza na mwenzi wako kwa sauti ya kubembeleza, ukamuuliza jinsi siku yake ilivyokuwa, ukampa pole kwa majukumu ya kutwa nzima. Mazungumzo ya namna hii huwaweka karibu zaidi wanandoa kimwili na kihisia.

KUKOSA KAULI NZURI

Nimewahi kupata malalamiko kutoka kwa mdau mmoja ambaye alisema mwenzi wake amekuwa na tabia ya kumjibu kwa mkato, kumtolea lugha chafu au kumfokea hata katika muda ambao hakuna alichomkosea.

Matokeo yake, ule uchangamfu kati ya mtu na mwenzi wake unapungua na kuendelea kufifia kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele, baadaye unaanza kumuona mwenzio kuwa mtu wa kawaida, hisia za mapenzi zinapotea kabisa. Hata kama umejizoesha muda wote kuwa ‘serious’, jitahidi kufurahi na mwenzi wako japo kwa dakika chache kabla ya kulala, hii itaongeza ukaribu kati yenu.

KUKOSA USAFI WA MWILI

Baadhi ya wanandoa, wakishaanza kuishi maisha ya wawili, hujisahau hata katika yale mambo ya msingi yanayoweza kuboresha mapenzi. Unakuta mtu anapanda kitandani akiwa mchafu, mwili unatoa harufu za ajabu, kikwapa kinanuka, harufu kali inatoka mdomoni na vitu vya namna hiyo. Unafikiri mwenzi wako atavutiwa kukumbatiana na wewe au kuzungumza kimahaba? 

Utakuwa kero kwake na atatamani kila mmoja angekuwa na kitanda chake. Kama wewe ni mwanamke, hakikisha ukishamaliza majukumu yako ya kutwa nzima, unatenga muda wa kuoga vizuri na kujipamba, kama una manukato huo ndiyo muda wake.

KUWA NA VISINGIZO VINGI KUHUSU TENDO

Upo ushahidi wa wanandoa ambao wana kawaida ya kukwepa kuwapa wenzi wao haki ya ndoa wanapohitaji. Yaani muda wa kulala ukifika, yupo radhi hata achukue nguo akaanze kufua ili akirudi akute mwenzi wake ameshalala. Mwingine anajifanya yupo bize na kazi za ofisini ilimradi tu hataki kuguswa na mwenzi wake.

Hakuna kosa kubwa linalosababisha ndoa nyingi kuvunjika kama wanandoa kushindwa kutimiziana haja zao za msingi hususan katika tendo la ndoa.

Kama kuna jambo limesababisha ukakosa hamu ya kukutana na mwenzio ni bora mkajadiliana kwa upole na kutafuta namna ya kulishughulikia kwa sababu wakati mwingine, baadhi ya wanandoa hukosa hamu ya tendo (hasa wanawake) kutokana na matatizo ya kisaikolojia au kimaumbile.

Kama hutaki kukutana naye kwa sababu unajua atakuacha njiani kama alivyofanya juzi na jana, kumkwepa siyo suluhisho bali mnaweza kukaa na kulizungumzia tatizo lililosababisha ukawa na hali hiyo. Yapo malalamiko ya baadhi ya wanaume kwamba wake zao hawaishi visingizio linapokuja suala la kuwa faragha, asiposema anaumwa kichwa basi atasema anaumwa tumbo au amechoka.

Matokeo yake mnasababisha ufa na baadaye mmoja anaona ni bora atafute mchepuko wa kumtuliza kuliko mateso anayoyapata ndani kwa kulazwa na njaa kila siku.

KWENDA KULALA UKIWA NA HASIRA

Hakuna kitu kibaya kama kupanda kitandani huku ukiwa na hasira, iwe aliyezisababisha ni mwenzi wako au ni mtu mwingine yeyote. Wapo baadhi ya watu ambao kwa sababu siku hiyo alifokewa na bosi wake kazini, basi kutwa nzima anashinda akiwa na hasira na hata muda wa kulala ukifika, anapanda kitandani akiwa na kisirani.

Wachambuzi wa masuala ya mapenzi, wanaeleza kuwa hii ni sumu mbaya ambayo kama unaipenda ndoa yako ni lazima upambane kuhakikisha unaachana nayo. Kuna usemi maarufu usemao, yaache matatizo ya kazini kwako kazini na yaache matatizo ya nyumbani kwako nyumbani.

Hata kama siku yako ilikuwa mbaya ni makosa kwenda kummalizia hasira mwenzi wako. Pia kama mwenzi wako ndiye aliyesababisha uwe na hasira, usikimbilie kwenda kulala na hasira zako ukidhani kwamba hilo ndiyo suluhisho. Hata kama umekasirika kiasi gani, jipe muda wa kutulia kisha zungumza na mwenzi wako kuhusu kilichosababisha ukakasirika.