ufahamu kwamba si kila mwanaume unayekutana naye na ukampenda anafaa kuwa mumeo. Wengine wana mapungufu makubwa ambayo bila kuyabaini na ukaingia kichwakichwa, utakutana na matatizo makubwa.
Kwa maana hiyo basi, sifa hizi sita ambazo nitazizungumzia leo endapo utaziona kwa huyo ambaye macho yako yameganda kwake, fanya maamuzi sahihi ya kumkubalia.
1.Anakupenda kwa maana ya kukupenda
Unapoingia kwenye maisha ya ndoa, unatarajia kupata mapenzi ya kweli kutoka kwa mwenza wako. Wapo wanaume ambao wanaonesha wazi kutokuwa na mapenzi ya kweli bali wanakuwa na mapenzi ya kuzuga.
Wanachotaka wao aidha kupata umaarufu tu kwamba yuko na demu flani bomba au kuonja tu penzi kisha kuanza visa ili muachane.Kwa nini ni vizuri kumpata mwanaume mwenye mapenzi ya dhati? Hii inatokana na ukweli kwamba kinyume na hivyo, maisha yatakuwa ya migogoro kila siku. Atakufanyia mambo ya kukuumiza kwa kukusaliti bila kujali maumivu utakayopata. Hii yote ni kwa sababu hana mapenzi ya kweli na wewe.
Ndiyo maana unashauriwa kwamba, kabla hata ya kumuonjesha penzi kisha kufanya maamuzi ya kumruhusu aende kwa wazazi wako ili mfunge pingu za maisha, ni vyema ukawa na uthibitisho kwamba anakupenda kwa moyo mmoja.
2.Hili la tabia ndo’ kila kitu
Linapokuja suala la ndoa, tabia inakuwa kitu cha awali sana kuangaliwa. Hii ni kwa sababu, wapo wanaume ‘handsome’, wenye kazi nzuri na kipato kizuri lakini wanakosa sifa ya kuitwa mume kutokana na tabia zao chafu.
Hakuna mwanamke anayeweza kudiriki kumpa nafasi mwanaume kuwa mume wake wakati ana tabia chafu. Endapo utaangalia uzuri wa sura kisha ukafanya maamuzi ya kuolewa naye, utakuwa umejichimbia kaburi.
3.Awe anaota mafanikio
Hivi karibuni kumekuwepo na mabadiliko ya aina yake kwa wanawake. Wengi hawapendi kabisa kuolewa na mwanaume ambaye hana kazi.
Mwanaume anatakiwa kuwa dereva katika safari ya kusaka mafanikio, sasa kama atakuwa ni mtu wa kukaa kijiweni, kupiga mizinga, mvivu asiyependa kujishughulisha kwa namna yoyote, huyu hafai kupewa nafasi ya kuitwa mume.
Ile dhana ya kukubali kuolewa na mwanaume yoyote ili mradi upate heshima ya kwamba umeolewa, imepitwa na wakati. Mwanaume sahihi ni yule mwenye malengo maishani, anayefikiria nini cha kufanya kwa ajili ya maendeleo yake, mkewe na watoto wao.
4.Wa shida na raha
Wapo wanaume ambao siyo wavumilivu kabisa katika maisha.Tunajua maisha siku zote hayatabiriki, yanaweza kutokea matatizo ya kiafya ama kifedha.
Kwa mfano, unaweza kuingia kwenye maisha ya ndoa lakini kwa bahati mbaya ukawa huna kizazi, mwanaume mwenye mapenzi ya kweli na wewe anatakiwa kukuvumilia na kuwa upande wako.
Yule ambaye atakuwa anaungana na dada zake kukushambulia kwa kutozaa, hafai kuwa na wewe kwani yapo mengi yanayoweza kutokea yanayohitaji kuvumiliana.
Kimsingi uvumilivu kwa mwanaume utakuwepo kama tu atakuwa na mapenzi ya dhati kama nilivyozungumza hapo awali. Mwanaume mwenye mapenzi ya dhati ni lazima atakuwa mvumilivu na atakuwa tayari kuishi katika maisha ya aina yoyote, yawe ya raha ama ya starehe.
5.Anayejua thamani ya mke
Wapo wanaume ambao hawajui thamani ya mke na ukiwachunguza utabaini hawafai kuwa waume za watu. Mume sahihi ni yule anayejua kwamba mke ni kitu cha faraja kwenye maisha yake.
Yule anayeamini kwamba, bila mke maisha yake hayawezi kuwa yamekamilika. Wapo ambao wanaamini hata bila wanawake wanaweza kuwa na maisha mazuri.
Mwanaume mwenye dhana hii, ukimpa nafasi kwenye moyo wako na ukaingia naye kwenye maisha ya ndoa, lazima atakuwa mguu ndani, mguu nje. Hataona hatari kukupa talaka hata kwa jambo dogo tu ambalo mnaweza kuongea na mkalimaliza.
Ndiyo maana nikasema, mwanaume sahihi wa kumpa nafasi ya kuwa mumeo ni yule anayejua thamani ya mke, anayeweza kuvumilia yote akijua mke ndiye anayekamilisha maisha yake.
6.Asiye na tamaa za kijinga
Unaweza kuwa na mpenzi wa kawaida ukiwa na malengo ya kumfanya awe mumeo katika siku za baadaye. Huyu ukigundua ana tamaa, huna sababu ya ‘kumpetipeti’.
Wanaume wenye tamaa za kijinga ndiyo ambao wakishaingia kwenye maisha ya ndoa wanakuwa wepesi kusaliti. Hao hawastahili kuitwa waume za watu.
Mwisho kabisa naomba niseme kwamba, licha ya sifa hizo 6, yapo mambo mengine ambayo ukiyaona kwa mwanaume ambaye ulikuwa unahisi anafaa kuwa mumeo, ni vyema ukapingana na mawazo.
Mwanaume asiyepitwa na sketi, asiyependa kumsikiliza mwenza wake, anayependa kufanya maamuzi bila kutaka kumshirikisha mwenza wake, anayekuwa upande wa ndugu zake unapokuwa kwenye matatizo, asiyejali familia yake, anayekuona wewe si lolote, asiyethamini na kuwaheshimu ndugu na marafiki zako, huyo kaa naye mbali kabisa.