Tuesday, June 12, 2018

Magonjwa Hatari Yatokanayo na Kujamiiana !

Nitakuwa nayachambua magonjwa mbalimbali hatari yatokanayo na kujamiiana ambayo kitaalam huitwa Sexually Transmitted Diseases (STD) ili tuweze kujiepusha nayo na wale ambao wanasumbuliwa na magonjwa hayo waweze kuyatibu na kujiepusha kuwaambukiza wengine.
Ifahamike kuwa magonjwa yote ya zinaa huathiri wanawake na wanaume lakini baadhi ya magonjwa hayo huwa na madhara zaidi kwa wanawake, hii ni kwa sababu pale mjamzito anapokuwa na ugonjwa wa zinaa, baadhi ya magonjwa hayo huweza pia kumuathiri mtoto atakayezaliwa.
Kati ya magonjwa yanayoathiri watu wengi duniani ni magonjwa ya zinaa. Haya ni magonjwa yanayoambukiza kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kupitia vitendo vya ngono.
Vitendo hivyo vya ngono ni kujamiiana, vitendo vya ngono kwa kutumia mdomo (oral-genital sex), kujamiiana kupitia njia ya haja kubwa (anal sex) iwe kwa mwanaume na mwanamke au kati ya wanaume wenyewe na hata wale wanaotumia vifaa vya kufanyia ngono (vibrators).
Magonjwa ya zinaa huathiri zaidi watu walio na umri wa kati ya miaka 15 hadi 30 lakini pia yanashuhudiwa kwa wingi kwa watu wengine walio na umri wa chini au zaidi ya huu niliotaja.
Kuna magonjwa ya zinaa zaidi ya 20 yanayotambulika duniani, yakiwemo haya:- Kisonono au gono (Gonorrhoea), Chlamydia, Kaswende (Syphillis), ugonjwa wa zinaa unaoambukizwa na Virusi vya Human Papilloma (HPV), Ukimwi yaani Upungufu wa Kinga Mwilini au HIV/AIDS na kadhalika.
Upo pia ugonjwa wa zinaa unasababishwa na virusi aina ya Herpes au Herpes Virus, Trichomoniasis, ugonjwa wa zinaa unaoambukizwa na bakteria yaani Bakteria Vaginosis, chawa kwenye nywele sehemu za siri na Chancroid.
Tunapaswa kufahamu kuwa magonjwa mengi ya zinaa au STD’s yanatibika lakini kuna baadhi ambayo hayana tiba kama vile Ukimwi, HPV nk.
Sababu zinazofanya watu kupatwa na magonjwa ya zinaa hufanana, kwa hivyo hapa tutaashiria kwa jumla visababishi vya magonjwa ya zinaa.
Kuanza vitendo vya ngono mapema au wakati wa umri mdogo au kuwa na wapenzi au washiriki wengi wa ngono, tukimaanisha kufanya ngono na watu tofauti ni moja ya sababu ya watu kuambukizwa maradhi haya.
Kufanya ngono zisizo salama au ngono zembe pia huchangia kusambaa kwa magonjwa haya.Maambukizi kupitia michubuko au sehemu zilizokatika kwenye ngozi kwa kugusana na majimaji ya aina yoyote kama damu, mate na kadhalika yanayotoka kwa mtu mwenye ugonjwa wa zinaa ni sababu ya kuenea magonjwa haya.