UNAWEZA kuambiwa maneno mengi sana kutoka kwa mpenzi wako, mazuri na mabaya lakini yapo ambayo yanatoa taswira isiyo nzuri. Jambo la msingi ni kuwa makini kupambanua.
Pointi ya msingi hapa ni lugha zenye ishara mbaya kwa wapenzi. Umewahi kujiuliza kuhusu hili? Umewahi kutafakari juu ya kauli chafu anazotoa mpenzi wako dhidi yako?
Hapa nimekuandalia kauli zenye ishara mbaya ya penzi lako. Ukiona moja kati ya kauli zifuatazo, basi kuwa na mashaka, kisha fanyia kazi, utagundua ukweli.
AKIKUAMBIA HUVUTII!
Kati ya kauli mbaya zaidi katika uhusiano ni pale mpenzi wako atakapokuambia huna mvuto! Haijalishi amekuambia akiwa katika hali gani; utani au akimaanisha, lakini neno hilo si zuri kuambiwa na mpenzi wako.Kuambiwa huvutii, katika mapenzi ni tusi kubwa. Nini maana ya mvuto basi? Nani umvutie? Ni wapita njia? Ofisini? Sokoni? Ana maana gani hasa?
Siku zote mvuto ni kwa ajili ya mpenzi wako, ndiyo maana mkawa katika uhusiano, hii inamaanisha ulimvutia ndiyo sababu akakukubali. Kukuambia huvutii si utani, ni kweli haoni mvuto na inawezekana penzi limeshachuja.
Inawezekana akawa anafanya mzaha, kama ndivyo, atasoma ulivyopokea, akiona umekasirika atarekebisha usemi wake haraka, kama ni vinginevyo ataendelea kushikilia msimamo wake, hata kama ni kwa utani, lakini atakuwa anakufikishia ujumbe wako kwamba huna mvuto, kwa maneno mengine humvutii, humfai; kwa hiyo muachane. Kuna nini tena hapo? Akili kichwani mwako.
ETI HUPENDEZI!
Hii ni kauli nyingine mbaya. Unapoambiwa: “Hujapendeza kabisa, yaani huna uwezo wa kupangilia nguo, kila siku unachemsha!” Ujue kuna hatari hapo, angalia mara mbili uhusiano wenu.
Kuambiwa hujapendeza kunashusha thamani yako na kuonekana huna ujanja wa kufanya uchaguzi mzuri wa mavazi. Huenda ni kweli hujapendeza, lakini hilo si la kubeza.
Anatakiwa kukuambia kwa upole namna ambavyo unatakiwa kuvaa na kuonekana nadhifu. Kwa maneno mengine, kukuambia hujapendeza ni kama anakusuta, hakukubali na unamuaibisha!
Bado kuna mengi ya kujifunza zaidi lakini kutokana na ufinyu wa nafasi yangu, naomba niweke kituo kikubwa hapa, wiki ijayo tutaendelea, USIKOSE!