Monday, May 14, 2018

Pete ya Uchumba si Ndoa, Je mwanamke unajua hiyo ni nini?


Rafiki zangu leo tutajifunza kitu kipya kabisa. Naamini utabadili namna ya kufikiri mara mada hii itapofika ukingoni. Nazungumzia kuhusu pete za uchumba. Hizi zimekuwa maarufu sana katika jamii yetu siku hizi.

Watu wanakutana disko, wiki mbili baadaye wanavalishana pete! Tayari ameshachumbiwa na amekuwa chini ya miliki ya mtu. Uko wapi usahihi wa pete za uchumba? Vijana wamechanganyikiwa kwelikweli! Wanataka pete tu!

Inawezekana wewe msichana unayesoma mada hii sasa hivi umevaa pete ya uchumba au pengine uko njiani kuvalishwa...vizuri! Lakini unaelewa nini kuhusu pete ya uchumba? Unautumiaje uchumba wako na mpenzi wako?

All About Love pekee ndiyo mahali utakapoweza kutolewa matongotongo kuhusu suala la pete. Nikuambie kitu? Usiniache please, twende pamoja tuone ukweli. 

NI NINI HASA?
Linatokana na neno la Kiingereza linaloandikwa engagement ring lenye maana nyingine ya commitment ring. Kwa Kiswahili rahisi ni pete ya ahadi. Msichana kuvalishwa pete ya uchumba, maana yake amevalishwa alama ya ahadi.

Jambo moja unatakiwa kusafiri nalo hapa ni kwamba, ahadi inaweza kutekelezwa au isitekelezwe.  

KUHALALISHA PENZI
Awali kulikuwa hakuna kabisa utaratibu huu wa pete za uchumba. Mvulana akimpenda msichana, taratibu za kawaida zilifuatwa kwa maana ya posa na baadaye mahari kisha ndoa. Hizi ni tabia za Kimagharibi ambazo zimekuja hivi karibuni.

Utaratibu huu umepokelewa vibaya (hasa na wasichana), wengi wamekuwa na shauku sana pete. Imani yao ni kwamba ukivalishwa tu, basi ndoa inanukia. Akipata mpenzi, anamlazimisha amvalishe pete.

Kwani kazi basi?! Aaah wapi! Jamaa anakwenda zake kwa Sonara anatengeneza pete ya laki tatu anamvalisha baa! Tayari wachumba! Hakuna mzazi wala mjomba anayejua. Hapo sasa ndiyo kwenye ukichaa – mwanamke atajiachia vyovyote atakavyo kwa mwanaume huyo.

Wanaume nao wanashangilia. Tatizo si pete? Anakuvalisha halafu anakutumia kwa nafasi, akiridhika anakuacha tena wengine huchukua na pete zao kabisa, halafu anatafuta mwingine anamvalisha. Mchezo unaendelea.

UCHUMBA SI NDOA
Dada zangu wapendwa fumbukeni macho, uchumba si ndoa. Utakuta mwanamke amevalishwa pete ya uchumba, basi kishakuwa mke. Atakwenda kwa huyo mwanaume, atafanya usafi, atafua, atapika na penzi atatoa!
Mwanaume anaridhishwa na kila kitu. Hapo unakuwa huna jipya tena. Hata kama anakupenda kwa kiasi gani, hawezi kuwa na haraka ya ndoa, maana kila kitu anachotakiwa kupata mwanandoa unampa!

Ya nini ajisumbue? Ya nini aanze kufikiria mambo ya vikao? Presha za nini? Haoni sababu na wakati muda ukizidi kwenda, anaendelea kukuchoka na kutafuta mwingine anayejitambua na kumuoa. Una lipi jipya utakalomwonesha ndani ya ndoa wakati kila kitu tayari anakijua?
Mabinti muwe makini. Kwa bahati mbaya sana, siku hizi wanaume wanakimbia kuoa mapema, ukijirahisi kwa pete utazivaa sana, lakini si ile ya madhabahuni. Utatumika na kuachwa.

UCHUMBA HUVUNJIKA
Acha kujidanganya, uchumba si ndoa (ingawa zipo zinazovunjika kulingana na ilipofungwa). Usiamini kuwa mchumba wa mtu basi kazi imeisha. Bado tena kubwa sana. Usikubali akutumie anavyotaka kwa kigezo cha pete.

Utakuta msichana amejitunza kwa muda mrefu sana lakini akishavalishwa pete tu, basi yupo tayari kwa lolote. Acha kujidanganya ndugu yangu. Endelea kujifunza na yeye anapaswa aendelee kukuheshimu kwa sababu bado si mke wake.
Baadhi ya madhehebu ya dini hutangaza ndoa kwanza kwa waumini kabla ya kufunga kwa sababu wanataka kupata uhakika wa wanandoa watarajiwa. Hata kama kanisani wanajua, kesho bwana harusi akikataa ndoa, hakuna wa kumlazimisha.
Kikitokea kipingamizi kadhalika, ndoa haifungwi tena. Kuwa makini.

UKWELI KUHUSU PETE
Achana na pete za kuvalishana uchochoroni. Mnavalishana pete gesti au kwenye kumbi za starehe – siyo sawa. Pete sahihi ni ile ambayo msichana atavalishwa mbele ya wazazi wa pande zote mbili, tena mahari ikiwa imeshatolewa na tarehe ya ndoa inajulikana.

Huu ndiyo usahihi na hapo tutakubaliana na wewe kwamba umevalishwa pete ya uchumba na upo mbioni kuolewa. Je, ukifikia hatua hiyo ndiyo ujiachie kwa mchumba wako? La hasha! Tena hapo ndipo unapotakiwa kuonesha heshima zaidi.

Kwamba wewe ni mchumba wa mtu na wazazi wako wanafahamu. Kuonekana mkiwa pamoja uchochoroni si kiashiria kizuri.  Je Kuna mahali nimekuacha? Nakupenda sana.


Usiache kusoma ukurasa huu wa Mapenzi  kuna mengi mazuri yanayokuja siku za usoni

Chears!

Makala hii imeandikwa na Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani