Monday, April 9, 2018

MAMBO 10 YA KUFANYA BAADA YA KUBAINI MPENZI WAKO AMEKUSALITI

MAMBO 10 YA KUFANYA BAADA YA KUBAINI  UMESALITIWA NA MPENZI WAKO! 
Karibu mpenzi  msomaji kwa kunitembelea katika blogi yangu, 
Leo napenda kushea nawe kitu muhimu katika maisha ambacho kinajitokeza mara kwa mara katika uhusiano na mahusiano kwa ujumla . 
Katika maisha ya kimapenzi hakuna kitu kinachouma kama kusalitiwa, tena kusalitiwa kunakouma zaidi ni pale ambapo unapobaini mpenzi wako amempa penzi mtu unayemjua halafu ukijilinganisha wewe na huyo aliyepewa unashindwa kuelewa kilichomshawishi mpenzi wako huyo kufanya hivyo.

Lakini licha ya kwamba usaliti si kitu kizuri, watu wamekuwa wakisalitiana, tena sana tu. Inafika wakati unashindwa kuamini kama yupo mtu ambaye hajawahi kumsaliti mpenzi wake.
Niseme tu kwamba wapo wachache waliotulia ila asilimia kubwa ya walio kwenye uhusiano na mahusiano ni wasaliti hata tafiti zimethibitisha hilo. Kama hali yenyewe iko hivyo, cha kujiuliza ni kwamba unapobaini mpenzi wako kakusaliti ni kipi unachotakiwa kufanya? Je, ni kuamua kunywa sumu kama ambavyo wamekuwa wakifanya wengine? Sidhani kama huo ni uamuzi sahihi. na mimi sikushauri hilo kabbissaa
Mtaalam wa masuala ya mapenzi James Johnson kutoka Marekani amependekeza mambo 10 unayoweza kufanya baada ya kubaini kuwa mpenzi wako amekusaliti.

1. Kubaliana na kilichotokea
Kama kishakusaliti ni tukio ambao limeshatokea na haliwezi kufutika. Kubali kuwa umetendwa, huzunika lakini mwisho liache lipite ili uweze kujipanga upya.

2. Usijilaumu
Wapo ambao wakishasalitiwa hujuta kukubali kuingia kwenye uhusiano na watu waliowatenda. Utamsikia mtu akisema ‘najuta kumkubalia awe mpenzi wangu’. Kujilaumu kwa namna hiyo hukutakiwi kwani kutakufanya uzidi kunyong’onyea.

3. Jitoe
Jifanye kama vile aliyesalitiwa siyo wewe bali ni rafiki yako kisha jiulize ungemshaurije? Ushauri ambao ungempata basi uchukue kisha uufanyie kazi.

4. Pima ulivyoathirika
Je, kitendo cha mpenzi wako kukusaliti kimekukosesha imani juu yake? Kama ni hivyo, unadhani una sababu ya kuendelea kuwa naye au unahisi madhara aliyokupatia huwezi kumvumilia?

5. Mpasulie ukweli
Kwa vyovyote utakavyoamua ni lazima umweleze juu namna alivyokuumiza kwa usaliti wake. Hata kama utampa nafasi nyingine lazima ajue jinsi alivyokuumiza ili iwe changamoto kwake.

6. Chunguza kwa nini kakusaliti
Usiliache likapita hivi hivi, unatakiwa kujua sababu ya yeye kukusaliti. Je, kuna ambacho anakikosa kwako au ni tamaa zake tu? Jibu utakalolipata litakusaidia katika maisha yako ya kimapenzi.

7. Usikubali akulainishe
Huenda huyo mpenzi wako ni ‘msanii’ na anaweza kukulainisha kwa maneno ambayo yanaweza kukufanya ukalichukulia tukio hilo kiurahisi. Kuwa na msimamo na eleza hisia zako kwa uwazi.

8. Amua kusuka au kunyoa
Likishatokea hilo jaribu kuzungumza na moyo wako. Uamuzi wa kuendelea kuwa naye au kumuacha uuchukue bila shinikizo. Hata kama kakuumiza, kama unadhani unaweza kumpa nafasi nyingine mpe ili usije ukajuta baadaye kwa kumkosa lakini kama unaona moyo wako unamkataa, muache.

9. Msamehe
Kwa uamuzi wowote utakaochukua ni lazima uwe tayari kumsamehe ili kuliondoa dukuduku lako rohoni. Kutokumsamehe kunaweza kukufanya ukawa unaumia kila wakati na kukosa amani.

10. Iwe fundisho kwako
Chukulia tukio hilo kama fundisho kwako. Huenda wewe ndiye uliyechangia kusalitiwa, kama ni hivyo badilika ili yasije yakakukuta kama hayo utakapokuwa na mwingine. Pia kama kusalitiwa kumetokana na kutoridhika kwa mpenzi wako, kuwa makini wakati wa kuchagua mwingine wa kuwa naye.