Zifuatazo ni baadhi ya dalili ambazo endapo mwanandoa atazibaini kwa mwenzake, anapaswa kuanza uchunguzi au kujadili naye jambo hilo ili kujiondoa katika wasiwasi. Lakini nitahadharishe kwamba dalili za mtu anayetoka nje ya ndoa ziko nyingi sana, kiasi kwamba siwezi kuziweka zote hapa, ila hizi nitakazozitaja zimethibitika kuwa zinapojitokeza, uwezekano ni mkubwa kwamba, mhusika anatoka nje ya ndoa yake.
1. Kuongeza upendo ghafla: mwanaume anapoanza kutoka nje yandoa, kama ndoa yake haina vurugu , anaweza kuonesha upendo mkubwa hadi mkewe akashangaa na kujiuliza . inakuwa kama vile ndiyo amekutana na mkewe kwa mara ya kwanza. Hii ni kutokanana kushitakiwa na dhamira kwa sababu anajua anachokifanya ni makosa huku akijua ndoa yake haina matatizo, na mkewe hajawahi kumkosea na anatimiza wajibu wake. Hata hivyo haina maana kuwa kila upendo ukiongezwa na mwanaume ghafla mwanaume huyo anatoka nje ya ndoa.Na ndio maana nikasema awali kuwa ni vyema uchunguze.
2. Kuona kasoro nyingi za mke: kama mume anaanaza kuona kasoro nyingi za mkewe ambazo hapo nyuma alikuwa hazioni, basi ana lake jambo. Hii ni katika kujitetea nafsini mwake, na kuhalalisha kwamba kutoka kwake nje kuna sababu
3. Mabadiliko ya kipato: Kuna wakati mabadiliko ya kipato yanaweza kuwa ni kiashirio cha mwanaume kutoka nje ya ndoa. Mwanaume anaweza kuwa na ajira ile ile au shughuli zilezile lakini ikaonekana kwamba kipato hakitoshi. Suala la fedha linaweza kuanza kuwa ni tatizo kubwa kwa familia.
4. Kujibadili sana: Ingawa siyo lazima, lakini hutokea wakati mwingine mwanaume ambaye ameanza kutoka nje ya ndoa kuanza kujibadili sana pia. Anaweza kuanza kuvaa nguo nzuri nzuri, kujipulizia manukato tofauti , kunyoa kwa mitindo tofauti na mengine yanayofanana na hayo. Mara nyingi mabadiliko hayo hufanywa na hiyo nyumba ndogo akijaribu kumbadili huyo mwanaume kwa kadiri anavyotaka yeye.
5. Alama na harufu mpya: Kama mwanaume siyo makini sana, kupatikana kwa rangi ya mdomo kwenye shati au nguo zake za juu ni rahisi sana. lakini hata kama ni makini, harufu ya pafyumu tofauti na ile anayotumia mkewe inaweza kusikika sana kwenye nguo zake.
6. Mazungumzo ya simu: Kama mwanaume anaanza kuzungumza kwenye simu kwa kukatishakatisha au kusema tu, nitakupigia baadae,' ama wakati mwingine kuonekana amebabaika baada ya kupokea simu, inaweza kuwa dalili. Kuna wakati anaweza kuwa anakata simu kila ikiita na kubadilika hata usoni kwa tahayari.
7. Ratiba ya kazi kubadilika: Kazi huwa inatumiwa kama kisingizio na wanaume wengi sana, hasa wanapoanza kutoka nje ya ndoa zao. Dalili kubwa kabisa ni ile ya mwanaume kuanza kuchelewa kurudi nyumbani kwa kisingizio cha kazi, kusafiri sana kwa kisingizio cha kazi, kulala nje kwa kisingizio cha kulala kazini (Night Shift).
8. Mbele ya wanawake wengine: Tafiti nyingi zinaonesha kwamba, wanaume huchukua wanawake ambao wako karibu nao, au wamewazoea kwa njia ya kukutana mara kwa mara. Ni rahisi mwanaume kuwa na hawara ambaye ni jirani, mfanyakazi mwenzie, mshiriki wake kibiashara, rafiki wa familia, au hata mwanafunzi wake. Kwa kawaida mwanamke mbaye anatembea na mume wa mtu anaweza kujionesha kirahisi anapokuwa na mwanaume huyo. Kwa hiyo mwanamke asijidanganye kwamba, kwa kuwa mwanamke fulani ni rafiki wa familia, ni jirani, ni mwanafunzi wa mumewe, hawezi kuwa na uhusiano naye, hapana. Kwa mwanaume, hao ni mawindo rahisi sana.