Friday, December 29, 2017

Ni rahisi sana Sana Kwa Mwanandoa Aliyeajiriwa Hapa Mjini Kuchepuka, Hivi Ndivyo Wanavyofanya

Nina uzoefu kidogo na mambo ya kazi za ajira maofisini, nimefanya hivi kwa muda mrefu. Wakati flani nilifanya kazi katika ofisi zilizo katikati ya jiji, kule mitaa ya Posta jijini Dar es Salaam.
Ofisi nyingi za serikali na watu binafsi zinapatikana mitaa ile. Kutokana na sababu hiyo, kuna idadi kubwa pia ya migahawa, hoteli, mama ntilie, pub na kadhalika.
Kuna mambo mawili makubwa yenye ushawishi mkubwa wa usaliti. Ofa za chakula au vinywaji na usafiri. Kwa kawaida, wafanyakazi wa ofisi moja hupenda kutoka pamoja wakati wa chakula cha mchana, wenyewe tunapendelea zaidi kusema lunch!
Kila mmoja ana sehemu yake anayokula kulingana na kipato chake, wapo wanaokwenda Southern Sun kupata chakula cha mchana, na wapo wanaowafuata mama ntilie wanaojibanza kwenye vichochoro vingi vilivyopo mjini.
Huko ndiko tunakokutana na akina dada waliovalia vizuri na kupendeza, wakitokea katika maofisi mbalimbali, huwezi kujua yupi ni mhudumu wa chai, yupi ni bosi, wote wanang’ara. Na hapa ndipo ofa za misosi zinapoanza kushawishi ngono.
Kijana mmoja mwenye kipato kikubwa ofisini kwake, atavutiwa na msichana mrembo mwenye mshahara wa wastani. Ili kumsogeza karibu, atalipia chakula cha siku hiyo na kumualika kwa kesho yake. Kulipiwa chakula ni jambo dogo, lakini lenye thamani kubwa sana. Si rahisi mtu aliyekulipia chakula kwa nia njema, ukaacha kumshukuru na hata kumwelekeza unapofanya kazi.
“Mimi nipo pale Oj Traders,” msichana anaweza kujita mbulisha jina na kusema anapofanyia kazi huku mkaka akimweleza kuwa yeye ni mhasibu katika ofisi flani. Watakapo
kutana mara ya pili, wataachiana namba za simu.
Baada ya hapo, mkaka atafanya mbwembwe za kuhamahama maeneo ya lunch ili mradi tu mdada wa watu aingie kwenye laini. 
Ukimaliza suala la lunch, kuna hii kitu foleni, hasa kwa wakazi wa Dar es Salaam. Raha ya kufanya kazi katikati ya jiji inaingia shubiri kadiri jioni inavyozidi kusogea. Kuanzia saa kumi, ni vurugu katika vituo vya daladala na hasa wakati kama huu ambao bodaboda zimezuiliwa kuingia mjini.
Wenye magari binafsi ndiyo wakati wao wa kujidai, ingawa foleni inawakumba wote. Lakini ni afadhali ukiwa kwenye foleni ndani ya gari dogo, mko wawili kuliko foleni, umeshika bomba kwenye daladala.
Siyo rahisi kwa mdada kukataa lifti ya kijana mwenye gari. Na katika foleni ndefu, ni wazi kwamba hadi mwisho wa safari, watakuwa wameshabadilishana namba. Kwa msichana, kuwa na uhakika wa usafiri kila siku ni ukombozi.
Tusidanganyane, hakuna msichana ambaye hatajua kuwa lunch au usafiri anaopewa unahitaji malipo maalum, ambayo ni penzi. Hali hii haiko Dar tu, bali nchi nzima na pengine duniani kote.
Mwanamke aliyeajiriwa anakuwa katika mitihani mikubwa zaidi ya kusaliti ndoa au uhusiano wake, kwa sababu hata kama haitakuwa kwenye chakula au usafiri, bado watu anaokutana nao katika utendaji wake, wanaweza kumghasi. Fikiria anakutana na mabosi, marafiki wa mabosi wake, wafanya biashara, atapona kweli?
Hata hivyo, simaanishi kama tabia hii inawakumba waajiriwa wote, isipokuwa nadhani ni sehemu kubwa wanahusika!