Saturday, December 2, 2017

KWA HALI ILIVYO SASA HIVI, HATA MPENZI WAKO HUENDA ANAJIUZA!

Mpenzi msomaji wangu, kichwa cha habari hapo juu huenda kimekushtua lakini huo ndiyo ukweli wa mambo! Nasema hivyo kutokana na kile ninachokishuhudia sasa hivi kwenye ulimwengu wa mapenzi.
Kwa wale ambao wanapitapita maeneo yanayosifika kwa biashara ya ukahaba watakubaliana na mimi kwamba hali ni mbaya sana. Mabinti wazuri sana wanaonekana mida ya usiku wakiwa mawindoni.Wanajinadi kwa wanaume wanaopita huku wakiwa wamevalia nusu utupu, lengo likiwa ni kupata pesa.
Katika wasichana hao ambao wengine hujiuza bila hata kwenda kusimama barabarani au kukaa kwenye kumbi za sterehe na baa, wapo ambao ni wake za watu na wengine wana wapenzi wao lakini wanajiuza kwa njia ya mtandao.
Swali la kujiuliza ni kwamba, inakuwaje mpenzi wa mtu anafikia hatua ya kufanya biashara hii haramu? Wakati unajiuliza hivyo, ufahamu kwamba wengi wanaojiuza wana tamaa ya pesa! Wanahisi kutokana na ugumu wa maisha, wanaweza kuitumia njia hiyo kujikwamua!
Sasa kwa hali hiyo kaa chini na ujiulize, unavyomuona mpenzi wako unahisi hana tamaa za kijinga linapokuja suala la pesa? Je, ni mtu anayeweza kukuvumilia hata pesa inapokosekana? Je, ni msichana ambaye hawezi kushawishika kirahisi?
Kama si mtu mwenye vigezo hivyo, ni rahisi sana kujiingiza kwenye biashara hiyo na wewe usijue.
Kuna mazingira f’lani ambayo yakiwepo kuna uwezekano mkubwa mpenzi wako akawa miongoni mwa wale wanaotumia miili yao kujipatia pesa.
Moja, kama mpenzi wako ana urafiki na wasichana ambao maisha yao yanategemea kuwezeshwa na wanaume, hata huyo wako anaweza kuingizwa huko.Wapo mabinti ambao wanajiuza lakini wana marafiki zao ambao ni wake au wapenzi wa watu. Sasa katika ongeaongea yao unaweza kushangaa changu anatoa ushuhuda kuwa biashara hiyo inalipa na ushuhuda huo ukimpata msichana asiyejua kuchuja mambo, unaweza kushangaa naye anaifanya kwa siri.
Mifano ya watu hao ipo, wapo ambao walikamatwa wakijiuza tena wengine wakiwa wana kazi zao lakini wakajitetea kwamba wasitolewe magazetini kwa kuwa wapenzi/waume zao wakiona itakuwa aibu. Hiyo inaonesha wazi kwamba, miongoni mwa watu wanaofanya biashara hiyo ni wale walio kwenye uhusiano, ndiyo maana nikasema hata siku ukitonywa kuwa mpenzi wako anajiuza, usikatae bali fanya uchunguzi kwanza.
Pili, kama wewe unajua kabisa kwamba mpenzi wako ana tamaa ya kupenda kuvaa vizuri, kuwa na simu kali, kula chakula kizuri na kuishi sehemu nzuri kisha wewe ukawa humpatilizi, ukijipindua kidogo tu unaweza kukuta anatumia njia zake anazojua ikiwemo hii ya kujiuza kupata pesa.
Lakini pia ukiwa na mpenzi kisha ukawa mgumu kumsaidia katika yale ya msingi wakati uwezo unao, unamshawishi kujiuza. Ndiyo maana niliwahi kusema kwamba, ubahili wako unaweza kumfanya mpenzi wako licha ya kukupenda akatafuta mtu kama siyo watu wa kumuwezesha.
Kutokana na hali hiyo nilisema kwamba, unapoingia kwenye uhusiano na mtu, hakikisha unamuepusha na vishawishi vya kujiuza, kupapatikia wanaume wenye pesa, kupenda starehe wakati uwezo haupo.Haya mambo jamani yapo, wapo wake za watu ambao wanaachwa nyumbani na waume zao lakini wana wanaume kibao ambao huwasiliana na kuwapa huduma kwa malipo tena kwa siri kubwa.
Utashangaa hata ukiwa na hali ngumu kifedha, mnakula vizuri, anajinunulia nguo za bei mbaya kila wakati na wala husikia akikulilia kwa shida ndogondogo. Unadhani katika mazingira hayo siku ukiambiwa mkeo anajiuza utakataa? Najua huwezi kukataa kutokana na mazingira ambayo umekuwa ukiyaona. Hivyo ni jukumu letu sisi tulio kwenye uhusiano kuwa makini na wapenzi wetu.
Tuna jukumu la kuwapa elimu juu ya tabia hii ya kutafuta pesa kwa kutumia miili yao na kuwaeleza wazi kwamba, wengi waliokuwa wanafanya kazi hiyo leo hii wamekufa na wengine wanaishi maisha ya tabu kufuatia kuambukizwa virusi vya Ukimwi au wameanza kuugua maradhi hayo.