Thursday, December 28, 2017

About Love; Je Unafahamu Dawa Ya Kutendwa ? Soma Hapa

HABARI zenu wapendwa wasomaji wa safu hii. Nimefurahi tumekutana tena kwa mara nyingine ili kupeana mawili matatu yanayohusu mahaba, hasa kwa kuwa baada ya kazi ngumu za kujenga taifa letu, tunahitaji nafasi kwa ajili ya kupumzisha mwili kiakili.
Juzi nilikuwa na rafiki yangu mmoja tumekaa sehemu tunabadilishana mawazo, akanipa simulizi ambayo imezaa mada hii. Alinisimulia mkasa wake kuwa anahisi mke wake anatoka na mtu mwingine, kwa sababu baada ya kuishika simu yake kwa siri na kuipekua, alikutana na baadhi ya sms zilizompa utatanishi kidogo, ingawa alishindwa kujiridhisha moja kwa moja kuwa zilikuwa zinatoka kwa mwanaume.
Baada ya kukutana na tukio hilo, kwa sababu alishindwa kumuuliza mkewe kwa hofu ya kuonekana kupekuapekua simu yake, basi alichofanya ni kumkumbuka mmoja wa michepuko yake kisha akapanga naye kukutana sehemu ili kuondoa stress.
Hapo ndipo nilipojikuta nabaki hoi, kwani aliniambia kila mara inapotokea hali kama hiyo, anachofanya ni kutoka nje ya ndoa yake na akishafanya hivyo, roho yake hubaki kwatu. Sababu kubwa ya kufanya hivyo, kwa mujibu wa maelezo yake, eti kama mbwai na iwe mbwai tu.
Ingawa nilimsikiliza na kumwelewa, lakini sikutaka kumuacha aendelee kuwa na tabia hiyo, siyo kwa uwezekano wa magonjwa ya zinaa, bali kisaikolojia, akili yake anaiweka katika sehemu ambayo haimsaidii.
Dawa ya kupigwa ngumi haiwezi kuwa kurudisha ngumi kwa sababu ugomvi hautakwisha. Ili kuondoa ngumi, ni lazima kukaa na anayekupiga ili kujua sababu ya kukupiga, maana huenda unafanya kosa bila wewe kujua kama unakosea.
Unajaribu kujiuliza, kama mke atapata hisia za kusalitiwa na mume wake, halafu na yeye akatoka nje ili kulipa kisasi, hii itakuwa ni ndoa ya aina gani?  Yaani watu hao wawili wakihisiana tu, ndani kumechafuka, kila mmoja anatoka kumtafuta mbadala!
Hivi itakuwaje kama ule mchepuko wako nao utakuletea za kuleta, kwa mfano na wenyewe ukagundua kwamba haujatulia, kwa hasira utakwenda kumtafuta mtu mwingine wa tatu?
Kama tunaamini katika mapenzi au ndoa zetu, basi dawa nzuri ya kuhimili kutendwa, ni kukaa na mwenza wako na kumueleza kwa uwazi kuhusu hisia zako, kwani hilo ndilo suluhisho la kudumu na tena lililo salama. Mwambie kuhusu ujumbe mfupi wa maneno ulioukuta katika simu yake, huenda anaweza kukuondolea hofu yako kwa kutoa ufafanuzi ambao utauelewa.
Watu wengi walio katika uhusiano au ndoa, hutikisa uhusiano wao kwa sababu ya hisia tu pasipo ukweli wowote. Ni kwa sababu tu amesikia akiongea na sauti ya kike au ya kiume, basi moja kwa moja huamua kuamini kuwa anayezungumza naye ni mpenzi wake.
Nimeshawahi kusema huko nyuma, kwamba hakuna raha katika uhusiano wa kimapenzi kama kujifanya kama vile humuoni mwenza wako na wala humfuatilii. Unampenda, lakini usiruhusu akili yako iumie juu yake. Achana na simu yake, mwache azungumze kadiri anavyotaka na wala usihoji kuhusu mwanamke au mwanaume uliyemuona naye.
Anayesaliti hujitambulisha mwenyewe, kama ni simu, ataenda kuongelea mbali na wewe ulipo, kama ni ujumbe wa simu, basi atakutazama kwanza kabla ya kujibu na vitu vingine kama hivi. Unapomtambua kwa dalili hizi, unamuumiza zaidi kama hutamuuliza kwa sababu hataelewa unachokiwaza moyoni mwako !
UMEICHEKI HII ? Diva Loveness Awapa Makavu Live Team Wema Sepetu ' Hamnilishi Hamnivishi Then My Life my Rule