Sunday, November 19, 2017



Wanawake wenye msongo wa mawazo “stress” huongezeka uzito kwa haraka sana kwasababu mfumo wao wa mmeng’enyo wa chakula “metabolism”kupunguza uwezo wa kufanya kazi. Mtikiso wa mawazo juu ya kazi yako, watoto wako, mpenzi wako, ndoa yako, mahusiano yako pamoja na marafiki zako vinatosha kabisa kukuletea msongo wa mawazo wa hali ya juu. Kwa msongo wa mawazo unaohusiana na mambo haya, wataalamu wanasema inaweza kukuongezea uzito wa hadi kilo 6.3 kwa mwaka.


Watafiti wa chuo kikuu cha Ohio huko Columbus Marekani walifanya utafiti uliowahusisha wanawake 58 ambao uzito wao wa wastani ulikuwa kilo 53. Kati ya maswali waliyoulizwa kwenye dodoso zao ni pamoja na kama kinachowapa msongo wa mawazo ni pale wanapowaza juu ya ndoa zao, wapenzi wao, marafiki zao, kazi zao, au watoto wao. Baada ya hapo wanawake hawa walipewa mlo wenye mayai, soseji, biskuti, nyama za bata mzinga n.k. Mlo huu ulikadiriwa kuwa na “calories” 930. Baada ya chakula hiki wanasayansi hawa wakawapima jinsi miili yao ilivyokuwa inasaga au kumeng’enya chakula na kiwango cha sukari mwilini mwao. Matokeo ya utafiti huu yalionyesha kwamba wanawake walioelezea kuwa na msongo wa mawazo kwenye kitu zaidi ya kimoja (baina ya watoto, kazi, ndoa, mpenzi au marafiki) waliweza kuchoma (kupunguza) wastani wa “calories” 104 pungufu ndani ya masaa 7 tofauti na wale ambao walionyesha kutokuwa na msongo wa mawazo (hapa inamaanisha uwezo wa mwili kuchoma virutubisho visivyohitajika mwilini ni mdogo sana kwa watu wenye msongo wa mawazo kuliko watu wasio na msongo wa mawazo). Kwa kipindi cha miezi 12 zaidi hali hii inaweza kusababisha ongezeko la uzito la hadi kilo 5 kwa mhusika. Wanawake wenye msongo wa mawazo wananafasi kubwa pia ya kuongeza kiwango cha sukari mwilini ambacho kinachangia pia katika kuhifadhi mafuta mengi mwilini. Zaidi ya hilo, wataalamu wanasema kwamba mtu mwenye msongo wa mawazo hushawishika zaidi kula vyakula vyenye mafuta mengi pamoja na vyakula vingine vyenye hatari kiafya, ambayo hii huongeza uwezekano wa uzito kuongezeka zaidi. Kiongozi wa utafiti huu Profesa wa saikolojia Jan Kiecolt-Glaser wa chuo kikuu cha Ohio anasema kwamba kwa kula vyakula vibaya kiafya kama vile vyenye mafuta mengi, vyenye wanga mwingi n.k uwezekano wa kuongezeka kwa uzito unakuwa mkubwa kwasababu miili yetu hupunguza uwezo wake wa kuchoma “calories” na hivyo kuchoma chache zaidi ya uwezo wa kawaida.


Mtaalam huyu ameeleza kwamba, ukiangalia chakula walichopewa wanawake hawa hakikuwa kibaya sana ukilinganisha na vyakula ambavyo wengi wetu tunakula pale ambapo tunaharaka ya kutaka chakula na hatutaki kupoteza muda kupika. Wengi wetu hatuko makini hata tunaponunua chakula au tunapokula kwenye sherehe mbalimbali, tunajitahidi kula kila kilichopo pasipo kuwa makini kwenye nini tunakula, kimepikwaje, kimepikwa na nini, na kipoje kuhusiana na afya yako. Watafiti hawa wamekiri kutokufahamu kuhusiana na hali ya mmeng’enyo wa chakula kwa wanaume hasa wanapokuwa na msongo wa mawazo. Wanahisi kwamba matokeo ya utafiti huu yanaweza yakawa tofauti kidogo kwa wanaume kwasababu wanaume wanamisuli. Hii inamaanisha kwamba mfumo wao wa mmeng’enyo wa chakula ni watofauti ukilinganisha na wanawake.
Tafiti nyingine zimeonysha kwamba msongo wa mawazo hutufanya tule sana hususani vyakula vya mafuta na sukari nyingi. Wataalam wanasema hii ni mbinu ya asili ya mwili kukabiliana na hofu au vitisho. Mtaalam wa lishe katika chuo kikuu cha Ohio Martha Belury anashauri kwamba ni vema tukaweka vyakula vyenye lishe na vilivyo bora kwenye makabati na majokofu yetu majumbani ili pale miili yetu inapotamani kuingiza chakula fulani, basi kinachopatikana kwa wakati ule kiwe chenye afya kwa mwili zaidi ya kuongeza kula vyakula vyenye athari kiafya.