Friday, November 24, 2017

MWANAMKE ANAHITAJI HAYA KUTOKA KWA MWANAUME

Habari yako rafiki yangu? Bila shaka u mzima kisawasawa, na ndiyo maana tu pamoja tena katika makala nyingine kutoka katika mtandao huu bora kabisa kwa ajili ya kushirikishana maarifa mbalimbali ya maisha. Kaa nami hadi tamati kuchota kitu kikubwa na chema kwa ajili ya maisha yako hasa katika suala zima la ndoa na mahusiano. 

Katika makala ya leo, nitakwenda kuzungumzia, mambo muhimu kabisa ambayo yatakusaidia kutunza ndoa yako; na kama bado hujaoa basi hii ni hazina yako ya kesho katika mahusiano. Wiki iliyopita nilieleza kwa umakini mkubwa juu ya nini ambacho mwanaume anahitaji kutoka kwa mwanamke. Hivyo, wiki hii, nimeona niandike makala mwenza wa ya ile wiki iliyopita kwa kuangazia upande wapili, yaani, nini ambacho mwanamke huhitaji kwa mwanaume.

Kama nilivyosema, zama za leo, maisha ya ndoa nyingi yanapita katika changamoto kubwa sana. Kiwango cha ndoa zinazovunjika kila kukicha kinaongezeka sana; na sababu kubwa ya ndoa hizo kuvunjiaka si nyingine bali ni wanandoa kutokuwa na maarifa. Watu wanaingia kwenye ndoa bila kufahamu misingi ya ndoa. Leo, ndoa za vijana, watu wazima, na vijana zinavunjika bila huruma na kuwaacha watoto wakiwa hawajui pakukamata.
Lakini, nikutie moyo kuwa kupitia mtandao huu wa Inuka Mtanzania, tutajitahidi kwa uwezo wetu, kwa sababu hilo ndilo moja ya dhumuni la kuuanzisha, kukufundisha na kuhakikisha unakuwa na maisha yenye mafanikio makubwa katika kila nyanja ya maisha. Kupitia mtandao huu utapata ujuzi mkubwa wa kutimiza ndoto zako katika biashara, huduma, ndoa, na kwenye maisha yako ya kiroho. Kwa hiyo endelea kuwa nasi kila siku, usikubali siku ipite hujatembelea mtandao huu kwa ajili ya kujifunza.
Kwa hiyo nikirejea kwenye mada yetu, yafuatayo ni Mambo muhimu ambayo mwanamke anahitaji kutoka kwa mwanaume:-

1.     Mwanamke Anahitaji Kupendwa.

Mwanamke anahitaji kupendwa, ninaposema kupendwa nina maanisha kupendwa kweli kweli. Ukitaka kumchukua mkeo mateka, wala huhitaji vitu vingi, wewe mpende tu, kisawa sawa. Zipo njia nyingi za kueleza upendo wako kwa mkeo, tafuta njia hizo na jifunze ili kuelezea hisia zako za upendo kwake, usikariri njia moja kila siku, jifunze kutumia njia mbalimbali kwa sababu ukitumia njia moja kila siku mwishoe ataikinai na itakosa maana.

Kuonyesha upendo kwa mkeo ni sawa na uwekezaji, maana mrejesho wa upendo umuonyeshayo utakurudia wewe tu maradufua zaidi. Kama hujui maana ya kupenda, ngoja nikusaidie, maana wengine kumpenda wanahisi ni kufanya tendo la ndoa, hapana, upendo ni kujitoa bila kujibakisha kwa ajili ya mwenzio; Mjali, mheshimu, mthamini, jitoe, na mfanye  kipaumbele katika yote unayoyafanya. Na wakati unafanya hayo usiwe unategemea chochote nyuma yake.
Mfanye mkeo kujiona wenye thamani kubwa katika dunia hii, mfanye kujiamini popote aendako. Ukimpenda mkeo huwezi kumuumiza kwa namna yoyote. Huwezi kutembea na mwanamke mwingine au kumdanganya, kila mara utamweshimu. Kuwa huru kuwa na mkeo, tembea na ye barabarani, usimfiche mkeo ndani tu, wanawake wanataka mwanaume anayejivunia kuwa naye. Usifanye siri kuwa naye kufanya hivyo ni kumfanya hajisikie vibaya.

2.     Mwanamke Anahitaji Mwanaume Anayempa Umuhimu.

Mwanamke anahitaji umuhimu kila mara uwapo naye, usimfanye mkeo kujiona yeye si muhimu kwako. Mfanye muhimu kwenye maongezi, kwenye shughuli  na kwenye mipango yako ya baadaye. Mwanamke hujisikia wa thamani sana pale anapoona unampa umuhimu kubwa katika shughuli zako. Usimpuuze, usimfiche siri zako kwa sababu huyo ndiyo mfariji na msaidizi wako, mweleze vyote kwa uwazi kabisa.

3.     Mwanamke Anahitaji Mazungumzo Na Mume Wake.

Mkeo anahitaji muda wa kuzungumza na wewe, kumbuka mwanamke huhamasika kwa yale anayoyasikia, tofauti na mwanaume ambaye huhamasika kwa yale anayoyaona. Kwa hiyo hapa ndipo unapoweza kumfanya mkeo kufurahia ndoa yake. Tenga muda zungumza naye kuhusu maisha yenu, mpe mpango au maono yenu baada ya muda fulani, mtie moyo na msifu pale anapofanya vyema. Kufanya hivi kutamsaidia mwanamke kufanya kilicho bora zaidi katika ndoa yenu.

Ukiweza kutumia vizuri mbinu hii ya mazungumzo utamfanya mkeo kuwa bora zaidi kwenye nyumba yako na atakuwa tayari kuifanya nyumba yako kuwa pepo itakayokusahaulisha mawazo ya kazi. Ongea na mkeo kwa upole, upendo na kwa umakini mkubwa. Mara zote penda kumsikiliza mkeo kwa umakini mkubwa, hakikisha anamaliza kuongea ndiyo na wewe ujiandae kumjibu, usimkatishe, au usiwe unafikiria jibu la kumpa kabla ya kumsikiliza mpaka mwisho, maana kufanya hivyo utashindwa kumuelewa alichokuwa anamaanisha.
Kama ulikuwa huwezi kuongea vizuri na mkeo, jifunze kuanzia leo kumsikiliza mkeo vyema na jifunze kumjibu kwa upole na upendo. Kama amekuudhi, jifunze kuwasilisha lalamo lako katika namna ya kumjenga na si kwa ukali kiasi cha kuchochea moto ndani yake. Pia iko hivi,  ujuzi huu wa maongezi unaweza kutumika kumwandaa mkeo kabla ya tendo la ndoa na mkeo akafika kileleni kwa furaha kubwa hujawahi kuona. 

Hivyo basi, tambua mwanamke anahitaji mwanaume aliye bora kabisa, na mwanaume aliyebora kwa mkewe ni mwanaume atakayeweza kuyafanya haya yote matatu tuliyojifunza hapo juu. Ukifanikiwa kuyafanya yote hayo kwa mkeo, utamtengeneza mwanamke wa ndoto yako.