natambua sana umuhimu wa mama katika jamii, na hata Mimi kabla ya hali ninayopitia nilikuwa napata homa hata tu nikisikia mama yangu yu mgonjwa ama anatatizo fulani, lakini hii haitoshi kunizuia kuelezea machungu anayonisababishia mama yangu tena mzazi, lengo langu hapa ni kupata msaada/ ahueni ya ninayoyapitia, inafika stage ninawaza hata kujitoa uhai lakini mungu yu mwema roho hiyo imekuwa ikishindwa.
Nilizaliwa katikati ya miaka ya themanini katika familia ambayo nilijikuta baba ni mtumishi wa serikali na mama ni mkulima, baba alitoka moja ya mikoa ya kanda ya ziwa kuja kufanya kazi mikoa ya nyanda za juu kusini, mimi nikiwa ni mtoto wa pili kuzaliwa kwa mama yangu baada ya Dada yangu huku baba akiwa na watoto wawili aliokuwa amepata kutoka kwa mke wa kwanza waliotengana.
Kumbukumbu nilizonazo ni maisha ya dhika, shiida na tabu tangu utoto huku migogoro ya baba na mama isiyoisha iliyokuwa inapelekea mara kwa mara mama yangu kurudi kwao yeye mwenyewe huku akituacha na baba ama tukienda pamoja, migogoro ya wana ndoa hawa kiukweli na pengine kwa sababu ya utoto hakuna aliyekuwa akijua nini chanzo chake na mwisho wake lini, ilifika kipindi hata kushikiana mapanga, visu ama mashoka ya nyumbani mbele yetu ilikuwa ni kawaida huku tukiishia kulia kwani tusingeweza kuamulia ugomvi na zaidi hata majirani walichoka.
Mwaka 1994 – 1995, baba yetu alikwenda kujiendeleza kimasomo kwenye chuo fulani kwenye mkoa huo, mama yetu kwa sababu alizozijua yeye huku akiwa na watoto sita aliamua kutoka pale alipotuacha baba na kwenda wilaya nyingine kupanga huku akisema hataki kuishi tena na MZEE,kwa hiyo akajichukulia mamlaka ya kubeba kila kitu na kwenda kupanga huku akifanya biashara ndogondogo na sisi tuliokuwa tukisoma akitutafutia uhamisho wa muda, hapa maisha haya kuwa rahisi, kuishi NYUMBA ya kupanga na watoto sita hata vitanda hakuna ni mikeka kutandikwa chini tu na wengine vikojozi du!!!!kwa kweli maisha haya sinta yasaha mbaya zaidi mbaya zaidi mbaya zaidi alikuwa anatuacha hata wiki mbili bila chakula cha kutosha akiaga kuwa anakwenda kwenye biashara huku baba yuko masomoni na hajui kama tumehama.
Baada ya baba kurudi toka masomoni na baada ya vikao vingi na virefu tukarudi tena makazi ya awali, 1996 baba aliamua kustaafu kwa hiari kwa mujibu ya sheria kipindi kile ilikuw ni miaka 50, hapo tukahamia mji mwingine ambako alikuwa amenunua uwanja awali, huko aliendeleza uwanja kwa kujenga nyumba kwa pesa za kustaafu huku akishindwa kuimalizia baadhi ya maeneo, Mimi nikiwa darasa la tano na dada yangu darasa la saba na wadongozangu wengine nyuma yetu, kiufupi hakuna aliyekuwa ameanza hata sekondari japo wale kaka zetu wa upande mwingine nao wakiwa hawajabahatika kuendelea na masomo, mmoja alikuwa nyumbani kwa akina baba na mwingine alifukuzwa Iyunga Tech kwa utovu wa nidhamu baada ya hapo akawa mtu wa stand hadi naandika hatujui yuko wapi hadi leo.
Kwenye makazi mapya maisha yalibadilika ghafla baada ya furaha ya muda mfupi, nyumbani paliendelea kuwa uwanja wa vita mbaya zaidi ugenini, baadaye mama akatoka mwaka 1999 akatengana na baba binafsi nikiwa ndo ninaelekea kumaliza darasa la saba na Dada yangu akiwa kamaliza na yupo nyumbani kipindi hiki ndo kipindi ambacho pengine kilikuwa na mateso zaidi kwani maisha yalikuwa magumu nyumbani hakuna chakula huku baba naye akishinda kusikojulikana lakini baadaye ikabainika kuwa alipata mke mwingine.
Ghafla mimi na mdogo wangu wa kiume aliyenifuata tukaingia kwenye kuhudumia familia, wakati huo pia baba alinipeleka kuanza kidato cha kwanza mwaka 2000 kwenye moja ya shule za sekondari za T.E.W.W, ada yake ikiwa Tsh. 35,000 kwa mwaka, hata hivyo pesa hiyo ilimshinda kulipa kwa wakati na hadi naacha 2002 baada ya shule hizo kufutwa na Mungai kulikuwa na deni kubwa.
Maisha yalikuwa magumu kweli kweli unaweza shinda njaa siku nzima hivyo tukaanza kuishi kwa udokozi, mfn. Tulikuwa na ng' ombe mmoja ambaye analishwa akiwa ndani hivyo tukienda kukata majani mimi na mdogo wangu lazima tuibe ndizi, mihog