Wednesday, November 15, 2017
JE,NIKIMPA HATANIKIMBIA?
Kaka asante sana kwa mafundisho yako na tunajifunza mambo mengi sana kuhusu ndoa na mahusiano.
Mimi ni mdada ambaye kweli Natamani kuolewa hata hivyo mchumba wangu anasisitiza kwamba tufanye mapenzi kwanza (sex) ili ajue nampenda.
Je, mapenzi kabla ya ndoa si ni jambo baya?
Dada asante kwa swali zuri na swali lako si mara ya kwanza kulijibu hapa hata hivyo kila siku tunajifunza kitu kipya.
Kwa ufupi ni kwamba kawaida mtu huhitaji kile ambacho hana.
Kama mchumba wako anakutaka kimapenzi (sex) kabla ya kuoana na wewe kwa ujinga wako ukamkubalia maana yake mkishamaliza kufanya mapenzi mwenzako atakuwa hana kitu cha kuhitaji kutoka kwako ili akuoe.
Umeshajiuza kwake kwa bei rahisi kabisa.
Kumbuka na fikiria upya, ukijirusha na mchumba wako kitandani hata kama mtakuwa mmejifunika shuka gubigubi ataona kila kitu mwilini mwako na atafahamu kila kitu kuhusu wewe.
Kwa mfano ataona alama mbalimbali mwilini mwako kama vile ukubwa wa matiti, chuchu, makovu ulivyonayo, tumbo, makalio, mapaja, sehemu za siri (kipara au msitu), mgongo wako, kiuno chako.
Atafahamu jinsi na namna unavyoguna kimapenzi, unavyobusu kwa kutetemeka, atajua harufu yako ukiwa uchi, atafahamu unavyolala kama gogo au ulivyo na kiuno kizito au ulivyo na aibu au ulivyo na maji au ukavu huko chini na mengine mengi.
Yaani ameona na uchi wako, una nini tena cha kumfanya akusubiri na kukuona special?
HUNA!
Kumbuka kwa kuwa anakutaka maana yake ameshatembea na mabinti wengi hivyo mambo yote nimeandika hapo juu atakuwa analinganisha na wale alitembea nao na kuangalia wewe umekuwa mshamba kiasi gani na kama anakuacha akuache lini.
Sasa hana shida tena kufikiria kuhusu wewe bali kukumbuka tu vile ulikuwa unafanya au ameona na anachofanya analinganisha na wanawake aliotembea nao na kuona wewe hakuna jipya cha maana ni kukubwaga chini na kutafuta mwingine.
Umeshaharibu maana ya vile alikuwa anategema kupata kutoka kwako au tuseme hana chochote cha kutegemea kutoka kwako maana umeshaonesha na kumpa kila kitu.
Kumbuka hana mkataba wowote na wewe na ana uhuru wa kukuacha kwani huna jipya kwake, hana kitu kinachomfanya ajisikie kukisubiri kutoka kwako maana anakujua ulivyo na Umeshajiuza kwa bei rahisi hivyo ana hiari ya kutafuta binti mwingine.
Mapenzi kabla ya ndoa ni dhambi, ni vibaya na ni sababu kubwa ya wengi kutooana na pia ni muhuri wa kukubaliana kwamba ndoa yenu haitakuwa na uaminifu.
Mchumba anayekutaka kimapenzi kabla ya ndoa mkimbie kwa kasi ya ajabu na usigeuke tena nyuma!