Sunday, November 19, 2017
JE UNAJUA CHANZO CHA HISIA GANZI ZA WANAUME KWENYE MAHUSIANO?
Tatizo kubwa la wanaume kukosa hisia na kushindwa kuzielezea au kuzionyesha hisia zao kwa wapenzi wao linachangiwa sana na makuzi na malezi, hapo zamani baba yake aliwahi kumwambia kuwa kuruhusu hisia zako zikajidhihirisha sio uanaume na labda mama yake akakazia kwamba ili kuwa mwanaume wa kweli lazima uwe mgumu, na mkakamavu kihisia, usije kukosa kuheshimiwa na mke wako. Hii inamfanya kijana wa kiume anakua akiwa na fikra kwamba hastahili kulia pale anapoumia moyoni, hastahili kusema chochote pale anaposikia kuumia kihisia na wala hana haja ya kushuka na kusema samahani, anabaki kuwa kama jiwe akizidi kuzifukia hisia zake na za wengine katika mambo mbalimbali. Kwa kushindwa kuzielezea au kuziweka wazi hisia zake mwanaume huyu anabaki kujifanyisha, kujilazimisha au kuzikandamiza hisia zake na kwa jinsi hii utamwona akionyesha ukali na vijihasira visivyo na sababu hali ambayo inaweza kuathiri sana mahusiano yake na mpenzi wake. Ewe baba na wewe mama, mfundishe mtoto wako wa kiume kuzionyesha na kuzielezea hisia zake katika hali njema na kwamba kuzionyesha hisia zake sio dhambi. Tuwajengee watoto wetu mazingira ya kuja kufurahia mahusiano yao na wapenzi wao huko mbeleni. Hata kama wewe hauyafurahii mahusiano yako na huyo mwenzako leo, usidhani na watoto wako pia hawana haki ya kuja kuyafurahia mahusiano yao baadae. “Be fair and be a parent, not just an adult with children”